Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutoa haki msingi katika udhibiti wa athari za mabadiliko
ya tabianchi
Mashirika mbali mbali ya Misaada na Maendeleo ya Kanisa Katoliki Kimataifa, yanasema
kwamba, Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoanza huko Doha, nchini
Qatar, kuanzia tarehe 26 Novemba hadi tarehe 7 Desemba 2012, iwe ni fursa ya kuweka
mikakati makini na endelevu ya kifedha inayolenga kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana
kikamilifu na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili hatimaye, kufikia muafaka wa
Kimataifa, ifikapo mwaka 2015.
Wajumbe wanapaswa kuweka mikakati ya haki, usawa
na inayotekelezeka pamoja na kutoa mbinu mkakati utakaotumiwa na Jumuiya ya Kimataifa,
ili kufikia malengo yatakayokuwa yamefikiwa, vinginevyo ni kupoteza muda na rasilimali,
wakati ambapo kuna maelfu ya watu wanaendelea kuathirika kutokana na mabadiliko ya
tabianchi.
Udhibiti wa madhara haya ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa, lakini
kwa namna ya pekee, Nchi zilizoendelea zinapaswa kuonesha mfano wa kuigwa kwa kupunguza
uzalishaji wa hewa ya ukaa inayotoka viwandani mwao, ambayo imekuwa ni chanzo kikubwa
cha athari ya mabadiliko ya tabianchi.
Mashirika ya Misaada na Maendeleo ya
Kanisa Katoliki Kimataifa yanasema, hadi sasa Itifaki ya Kyoto ndicho chombo pekee
kinachofanya kazi ya kudhibiti hewa ya ukaa, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita
zaidi katika utekelezaji wa malengo ya Itifaki hii itakapokuwa inaingia katika Awamu
ya Pili, hapo mwaka 2013.
Hadi sasa hakuna rasilimali wala utashi wa kisiasa
unaotaka kulivalia njuga tatizo la athari za mabadiliko ya tabianchi, wakati ambapo
kiwango cha nyuzi joto kinaendelea kuongezeka. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutekeleza
maamuzi yake. Ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi, vinginevyo, majanga
asilia yataendelea kusababisha umaskini, vurugu na kinzani za kijamii, kisiasa na
kivita.