Vijana wa Taizè kukutana Roma kuanzia tarehe 28 Desemba hadi tarehe 2 Januari 2013
Jumuiya ya Kiekumene ya Vijana wa Taizè kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Roma pamoja
na Idara ya shughuli za kichungaji kwa vijana, kuanzia tarehe 28 Desemba hadi 2 Januari
2013, watafanya mkutano wao wa thelathini na tano mjini Roma, kwa kuwashirikisha vijana
kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya, ambao watashiriki hija ya imani duniani.
Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa
hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Mkutano huu kwa namna ya
pekee, itakuwa ni fursa kwa vijana kujichotea utajiri wa upendo unaobubujika kutoka
katika tafakari ya kina na sala zitakazoendeshwa kwenye Makanisa Makuu yaliyoko mjini
Roma.
Ratiba inaonesha kwamba, tarehe 29 Desemba 2012, Jioni, Vijana wa Taizè
watakutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Vijana hawa ni kielelezo cha mshikamano wa
dhati unaofumbata tunu msingi za maisha ya kiroho, kama ilivyojionesha hivi karibuni
nchini Rwanda ambako vijana elfu nane na mia tano, kutoka katika nchi thelathini na
tano. Inawezekana kabisa watu wakaishi kwa umoja, upendo na mshikamano, licha ya tofauti
zao za kiimani.