2012-11-24 13:52:45

Kanisa ni: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, linapata chimbuko na hija yake kwa njia ya Umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu


Kanuni ya Imani inayoungamwa na Waamini katika Liturujia ni muhtasari wa Imani ya Kanisa ambayo kila mwamini anaipokea wakati anapobatizwa. Kwa kuiungama na kuilinda, waamini wanaweza kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo.

"Katoliki" ni neno linaloonesha umuhimu wa Kanisa na utume wake, kwani ni Yesu mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa lake kuwa ni: Takatifu, Katoliki na la Mitume pamoja na utekelezaji wake. Kanisa ni Katoliki kwani kwa njia yake, Yesu anawakumbatia binadamu wote katika utume wake kwa njia ya mwanga wa Injili unaoyaunganisha mataifa yote katika Ufalme wa Mungu. Huyu ndiye Mwana wa Daudi, lakini zaidi ni Mwana wa Mtu, kama anavyotambulikana katika Maandiko Matakatifu.

Hivi ni vielelezo makini anavyovitumia Yesu kuonesha utume wake wa kama Masiha wa ulimwengu wote. Kwa njia ya ubinadamu wake, anawavuta wote kuungana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa ambalo ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa kweli.

Hii ni sehemu ya tafakari ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyoitoa wakati wa kuwasimika Makardinali wapya sita katika Ibada iliyofanyika Jumamosi, tarehe 23 Novemba, 2012 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Yesu analituma Kanisa lake kwenda ulimwenguni kote, ili kuwaunganisha watu katika kifungo cha imani na hatimaye, kuwa ni Watoto wa Mungu, kama wanavyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Watoto hawa wanapaswa kujenga na kuimarisha umoja wao hadi pale utashi wa Mungu utakapokamilika.

Baba Mtakatifu anasema, Ukatoliki wa Kanisa unapata chimbuko lake katika Mpango wa Kazi ya Ukombozi wa dunia, hali ambayo ilijionesha kwa namna ya pekee, pale Roho Mtakatifu alipowashukia Wakristo wa Kanisa la Mwanzo, ili Injili iweze kuwafikia watu wengi zaidi, ambao wangefanyika kuwa ni Watoto wa Mungu, ndiyo maana hata Kanisa katika utume wake, linawakumbatia wote na kila mtu anaielewa lugha yake kama walivyoshuhudia Mitume siku ile ya Pentekoste.

Utume wa Kanisa la Kiulimwengu unapania kuunda umoja wa Watu wa Mungu, huku wakitoka kifua mbele kutangaza Habari Njema ya Wokovu, ili ufalme wa Mungu uweze kuwafikia wote. Kwa njia ya Roho Mtakatifu anasema Baba Mtakatifu waamini wamekirimiwa Mapaji ya Roho Mtakatifu, wakipewa wajibu na dhamana ya kumshuhudia kwa mataifa yote sanjari na kujenga ufalme wa Mungu.

Tangu mwanzo wa Kanisa, mitume na wafuasi wao hawakutegemea usalama katika nguvu za kibinadamu, bali waliongozwa na kutegemezwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, Injili na Imani, wakafanikiwa kuingia katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, lakini Kanisa daima likabaki kuwa ni MOJA. Makanisa mahalia yakaanzishwa na kuenea sehemu mbali mbali za dunia, lakini bado Kanisa likabaki kuwa ni Kanisa: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, linalopata chimbuko lake la maisha na hija yake kwa njia ya Umoja katika Fumbo la Utakatifu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, huu ndio mwelekeo wa Baraza la Makardinali, wanaoonesha sura tofauti za Kanisa, lakini wote kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kiulimwengu, ambalo ni la waamini wote kutoka katika mabara yote, kielelezo cha Kanisa la Pentekoste, linaloimba utenzi kwa Mungu aliye hai.

Baba Mtakatifu alitumia fursa hii pia kuwasalimia wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliofika mjini Vatican kushuhudia Makardinali wapya wakisimikwa rasmi, kielelezo cha mshikamano na ushirikiano wa kibaba na kirafiki; tayari wakiwa makini kutoa huduma yao ya kichungaji kwa Makanisa mbali mbali yaliyoko mjini Roma ili kuendelea kujenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo, kama walivyoapa katika kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Makardinali wanapaswa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo pamoja na Kanisa Takatifu. Wawe tayari hata kuyamimina maisha yao, kama inavyojionesha kwa njia ya Kofia Nyekundu za Kikardinali wanazovaa; lengo ni kueneza Imani ya Kikristo, kwa ajili ya kusimama kidete kuinda na kutetea amani na utulivu wa Watu wa Mungu.

Pete ambayo Makardinali wamevishwa na Baba Mtakatifu ni alama ya uaminifu na upendo wao kwa Kanisa; daima wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, kwani Kanisa la Roma ni kielelezo cha upendo wa Kanisa Katoliki. Watashirikiana kwa karibu zaidi na Mabaraza mbali mbali ya Kipapa na kwa njia hii, wanakuwa ni wasaidizi wake wa karibu katika kuchunga na kuliongoza kundi la Kristo kwa kuwa makini katika Mafundisho tanzu ya Kanisa, Nidhamu na Maadili.

Kwa njia ya karama na mapaji mbali mbali waliyokirimiwa Makardinali wapya, watachangia utajiri wa Kanisa la Kristo, daima wakijitahidi kutolea ushuhuda amini wa imani na huduma yao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.