2012-11-24 11:14:56

Baba Mtakatifu Benedikto XVI ametimiza ahadi yake!


Kitabu cha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuhusu Simulizi za Utoto wa Yesu, kimekuja kwa wakati muafaka, ili kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina hasa wakati wa Kipindi cha Majilio na Noeli, kinachotoa fursa maalum kwa ajili ya kuzama katika utamaduni wa Biblia; tafakari za kitaalimungu na maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu ametimiza ahadi ambayo alikuwa amejiwekea mwenyewe tangu alipochapisha kitabu chake cha kwanza kuhusu Yesu wa Nazareti, kinachofafanua kuhusu maisha ya Yesu hadharani; Kitabu cha Pili akazama zaidi katika Mateso na Ufufuko wa Yesu. Alikwisha sema wazi kwamba, lengo la kazi yake ni kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema, kuweza kumfaham zaidi Yesu; ujumbe na utekelezaji wa utume wake hapa duniani. Ndiyo maana aliacha kwa makusudi mazima, Simulizi za Maisha ya Utoto wa Yesu, ingawa aliweza kuwaonjesha wasomaji wake kidogo kuhusu maisha ya Utoto wa Yesu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatambua kwa unyenyekevu mkubwa kwamba, licha ya mapungufu yanayoweza kujitokeza katika kitabu hiki, lakini jambo la msingi ni kusaidia kujenga majadiliano ya kina kwa kuangalia yaliyopita, yaliyopo na yale yanayokuja kama hija ya watu kumwendea Yesu Kristo, ili kuandamana naye.

Ndivyo anavyoandika Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwenye tahariri yake juma hili, inayojikita katika ahadi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kutaka kuandika kitabu maalum kitakachogusa Simulizi za Utoto wa Yesu, ahadi hii sasa imetimia, kazi ni kwako mwamini. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, katika uzee wake, alijikita zaidi katika tafakari iliyoandikwa kwa mtindo wa shahiri juu ya "Utatu wa Roma".

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amejitahidi kuwasaidia watu wanaoutafuta uso wa Yesu ili kukutana naye. Alitambua vikwazo ambavyo vilikuwa mbele yake, vya kweli au kinzani zinazojitokeza katika tafakari ya kina katika Maandiko Matakatifu, Taalimungu, Utamaduni wa mwanadamu pamoja na kinzani binafsi.

Padre Lombardi anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameng'amua kwanza kabisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, jinsi ambavyo watu walijitahidi kumtofautisha Yesu wa historia na Yesu wa Imani. Amejibidisha kutoa mwelekeo wenye utulivu unaopania kujenga na kuimarisha urafiki binafsi na Yesu, huduma makini kwa viongozi wa Kanisa. Anatambua dhamana yake ya kulinda na kutetea Imani ya Kanisa.

Padre Lombardi, anachukua nafasi hii kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuweza kuhitimisha kazi kubwa ambayo imedumu kwa takribani miaka tisa. Hayati Kardinali Martini alipokuwa anahitimisha uzinduzi wa kitabu cha kwanza alisema kwa hakika, kitabu hiki ni kizuri, kinatusaidia kumfahamu Yesu Mwana wa Mungu na imani kubwa ya mtunzi wa kitabu hiki.







All the contents on this site are copyrighted ©.