2012-11-23 13:49:19

Utume wa Bahari: Onesheni ile sura ya Kanisa linalokarimu; zimeni kiu ya maisha ya kiroho ya mabaharia kwa ushuhuda wa maisha na tunu bora za Kikristo!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa, tarehe 23 Novemba 2012, amewashukuru wajumbe wa Utume wa Bahari waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa ishirini na tatu wa Utume wa Bahari, uliokuwa umeandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi.

Anasema, hii ni huduma ambayo imetolewa na Kanisa kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa na dini na imani zao; daima wakijitahidi kujenga na kudumisha moyo wa ushirikiano wa kiekumene na kidini.Mabaharia na Wavuvi pamoja na familia zao wanakumbana na hali ngumu ya maisha pamoja na changamoto mbali mbali zinazohitaji kuwa na mtazamo mpana zaidi wa tunu na maisha ya binadamu, mwelekeo ambao umeboreshwa kwa fadhila ya upendo.

Utume wa Bahari anasema Baba Mtakatifu una historia ndefu, kwani kunako Mwaka 1922 Papa Pio wa kumi na moja, alihidhinisha Katiba na Sheria, akawahimiza wahudumu wa maisha ya kiroho na watu wa kujitolea kupanua Utume wa Bahari, uliothibitishwa kwa namna ya pekee na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 75, kwa kuonesha utashi binafsi katika hati inayojulikana kwa lugha ya Kilatini: Stella Maris; yaani Nyota ya Bahari.

Katika mwelekeo kama huu, wajumbe wamechambua na kutafakari kuhusu dhana ya Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa mabaharia, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ili wafuasi wa Kristo, waweze kutambua na kujishikamanisha katika Injili.

Tangu mwanzo wa Ukristo, safari za baharini zimekuwa ni njia ya kutangaza Injili ya Kristo, utume ambao ulitekelezwa kwa namna ya pekee na Mitume wa Yesu, bila kusahau kazi kubwa iliyofanywa na Mtakatifu Paulo, mtume na mwalimu wa mataifa, changamoto inayoendelea kufanyiwa kazi na Mama Kanisa hata nyakati hizi kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu.

Ulimwengu wa mabaharia unakabiliana na changamoto zinazoibuliwa na utandawazi; kwa kukumbana na madhulumu; wanapotelekezwa na vyombo vyao; wanapotekwa nyara na maharamia baharini au wanapojikuta kwamba, wanalazimika kulipa gharama zinazotokana na uvuvi haramu. Mateso na mahangaiko ya mabaharia, wavuvi na wasafiri ni changamoto kwa Mama Kanisa, kuhakikisha kwamba, anawasaidia kwa upendo wake wa kimama, kwa njia ya wahudumu wa Utume wa Bahari.

Baba Mtakatifu anawakumbuka wavuvi na familia zao; kundi ambalo linaishi kwa wasi wasi na hofu kubwa kuhusu hatima ya maisha yao kwa siku za usoni, kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na uvuvi haramu. Anawahimiza wavuvi hawa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu wao kwa nidhamu na usalama, wakisimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kifamilia.

Watunze mazingira, utu na heshima ya kila mwanadamu; daima watambue kwamba, Kanisa liko pamoja nao kwa njia ya huduma za kichungaji zinazotolewa na Mashemasi wa kudumu; kwa kushirikiana na kusaidiana wao kwa wao, wakimtegemea Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wahudumu wa Utume wa Bahari, kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu kama wanavyosisitizia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika bahari ambayo wakati mwingine ina mawimbi makali au imetulia. Waendelee kukuza ndani mwao ari na moyo wa kimissionari, kwa kujenga na kuimarisha uhusiano mwema na Makanisa mahalia, kama njia ya Uinjilishaji Mpya kwa umati mkubwa wa watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao!.

Anawataka kuwa ni wachungaji waaminifu wa utume wa Kanisa katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kuonesha ile sura ya Kanisa linalokarimu sehemu hii ya Watu wa Mungu, kwa kuzima kiu ya maisha ya kiroho ya mabaharia kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya uhai wa Jumuiya inayoinjilisha!

Iwe ni fursa kwa kila mmoja wao kugundua uzuri wa imani, ili kuishuhudia kwa njia ya uhalisia wa maisha, Bikira Maria Nyota ya Bahari na Nyota ya asubuhi awaangazie katika huduma zao, ili mabaharia waweze kuifahamu Injili ya Kristo, wakutane na Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima.







All the contents on this site are copyrighted ©.