Nigeria tumieni vyema utajiri na urithi wenu wa kiimani kupambana na: ujinga, umaskini,
maradhi, rushwa na ufisadi!
Kardinali mteule John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, Alhamsi
tarehe 22 Novemba 2012 alipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari mjini Roma.
Pamoja na
mambo mbali mbali aliyoyazungumzia kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Nigeria,
ametumia fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuendelea
kuthamini ukomavu wa Kanisa Barani Afrika.
Hii ni changamoto kubwa kwa Kanisa
Barani Afrika kuhakikisha kwamba, waamini wanajenga na kuimarisha Kanisa ambalo limekita
mizizi yake katika Imani na ushuhuda wa maisha unaomwilishwa katika medani mbali mbali
mintarafu kweli za Kiinjili.
Kardinali mteule Onaiyekan anasema, Injili ya
Kristo inasimikwa katika misingi ya haki, amani na upendo. Huu ndio ushuhuda unaopaswa
kumwilishwa katika sekta mbali mbali za maisha na utume wa waamini Barani Afrika;
kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Akizungumzia kuhusu
hali tete nchini Nigeria, Kardinali mteule Onaiyekan anabainisha kwamba, usalama wa
raia na mali zao ni kati ya changamoto pevu nchini Nigeria. Hii inatokana na ukweli
kuhusu mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram, ambayo kwa
namna moja au nyingine yanafumbatwa katika masuala ya kidini. Hata katika mazingira
hatarishi kama haya Injili ya Kristo haina budi kutangazwa.
Ikumbukwe kwamba,
tangu mwanzo wa kuanzishwa kwa Kanisa limekumbana daima na madhulumu na kwamba, damu
ya Wakristo imekuwa ni chachu ya kukua na kukomaa kwa Kanisa ambalo linaendelea kufuata
nyayo za Muasisi wake, Yesu Kristo, aliyekabiliana na kifo uso kwa uso.
Dhuluma
ni nyenzo inayosaidia kukuza na kuliimarisha Kanisa, kumbe si bure hata kidogo! Jambo
la msingi ni kuhakikisha kwamba, katika kipindi hiki cha mpito Wakristo wanakuwa na
Imani thabiti na sahihi na wahakikishe kwamba, wanaishuhudia mahali popote pale walipo.
Kardinali
mteule anapenda kukazia: umoja, upendo, amani na mshikamano wa kitaifa na udugu, miongoni
mwa wananchi wote wa Nigeria. Licha ya tofauti zao za kidini, lakini kama raia wa
Nigeria kuna mambo mengi ambayo yanawaunganisha kwa pamoja, huku wakiendelea kuchota
utajiri na fadhila za kidini; ili wote kwa pamoja, waweze kusimama kidete kupinga:
ujinga, umaskini, maradhi na utawala mbaya; daima wakipania kutafuta mafao ya wengi.