2012-11-23 09:28:58

Mtumishi wa Mungu Maria Troncatti, F.M.A, kutangazwa kuwa Mwenyeheri


Katika shamra shamra za maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme, Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, atamtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Troncatti wa Shirika la Masista wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika huko Macas, nchini Equador, Jumamosi, tarehe 23 Novemba 2012.

Mwenyeheri Maria Troncatti alizaliwa tarehe 16 Februari 1883, Brescia, Italia. Kunako Mwaka 1905 akajiunga na Shirika la Masista wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo. Na Mwaka 1922 akatumwa na wakuu wake kwenda nchini Equador kama mmissionari. Akiwa huko alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wananchi wa Equador.

Alifariki dunia kwa ajali ya ndege tarehe 25 Agosti 1969, akiwa na umri wa miaka themanini na sita. Hata kabla ya kifo chake, watu wengi walianza kuonja utakatifu wa maisha yake, lakini umaarufu wake, ulianza kuenea mara baada ya kifo chake; baadhi ya watu waliomkimbilia kwa maombezi, wakasikilizwa katika shida na mahangaiko yao ndani.

Mwenyeheri Maria Troncati ni mwanga angavu wa utakatifu wa maisha katika nchi za Amerika ya Kusini, aliyejitofautisha na watawa wengine kutokana na fadhila zake katika maisha ya kiroho, pasi na makuu, mwenye imani thabiti na jasiri katika kutenda. Ni mtu aliyeboresha maisha yake kwa njia ya Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Yesu wa Ekaristi na kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Ni mtawa aliyejitoa kwa ajili ya utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro; akaonesha upendo wa kimama kwa watoto, wagonjwa, wajane, yatima, watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu pamoja na wahitaji; aliguswa na shida za watu mbali mbali, daima walimwona kama Malaika aliyekuwa anaishi kati yao! Alijitahidi kuokoa maisha ya watoto wengi kadiri ya uwezo wake. Alitolea ushuhuda wa Imani yake, ambao ulileta mguso kwa wananchi wengi wa Equador.

Ni mtawa aliyetumia muda wake mwingi kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Hata leo hii, anasema Kardinali Angelo Amato, Yesu anaendelea kuita vijana wengi, kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Ni changamoto kwa watawa wenzake kuhakikisha kwamba, wanamwilisha karama ya Shirika lao katika sekta ya elimu kwa vijana na watoto. Waamini wote watambue dhamana ya kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.