Maaskofu walaani vita na dhuluma inayoendelea nchini DRC
Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za Kanisa Barani Afrika katika mkutano
unaozungumzia utambulisho wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas, katika
ujumbe wao kwa Jumuiya ya Kimataifa wanasema kwamba, wanasikitishwa na mahangaiko
ya watu wanaokabiliana na vita mjini Goma, DRC na kwamba, kwa kauli moja wanalaani
vita hii ambayo haina tija wala mafao kwa wananchi wa DRC.
Vita hii imepelekea
watu wengi kuyakimbia makazi yao na hivyo kukabiliana na hali mbaya ya hewa, njaa
na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuwateka watoto
ili kuwapeleka mstari wa mbele kinyume cha sheria na kanuni za kimataifa. Vitendo
vyote hivi vinadhalilisha utu na heshima ya watu hawa ambao wamumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Caritas Goma inakisia kwamba, kuna zaidi ya watu laki moja ambao wamelazimika
kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Maaskofu kutoka Afrika
wanasema, huu si muda wa kupigana vita, bali kujenga mshikamano na ushirikiano wa
dhati miongoni mwa wananchi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa
DRC, kila mtu akiheshimiwa na kulindwa. Inasikitisha kuona kwamba, utajiri wa maliasili
badala ya kuleta mafao kwa wengi, umekuwa ukitumiwa na watu wachache kwa ajili ya
mafao yao binafsi.
Maaskofu wanasema, umefika wakati wa kuhakikisha kwamba,
kunakuwepo na usawa, haki na, ukweli na uwazi katika matumizi ya maliasili ya taifa,
ili iweze kuwa ni kikolezo cha maendeleo. Maaskofu wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba, pande zinazosigana nchini humo zinajikita katika majadiliano ili
kusitisha na hatimaye kukomesha kabisa vita nchini DRC na wahusika wafikishwe kwenye
mkondo wa sheria.