Hii ndiyo Imani Yetu inayosimikwa kwa Kristo na Kanisa lake!
Kardinali Jaime Ortega Alamino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Havana Cuba, katika maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, ameandika barua kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Havana, akionesha
umuhimu wa Imani. Anapembua kwa kina na mapana mwelekeo wa imani nchini Cuba kwa kuwataka
waamini kujikita katika kuifahamu, kuishuhudia na kuitetea imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake.
Anasema, katika ulimwengu wa utandawazi, watu wanaendelea kuonja
mtikisiko wa maadili na utu wema; watu wanatake kuishi kana kwamba, hakuna Mungu;
wakiongozwa na kusukumwa na mawazo mepesi mepesi bila ya kufanya rejea kwa Mwenyezi
Mungu ambaye ni muumbaji wa vile vinavyoonekana na vile visivyoonekana. Walimwengu
wanajidai kutaka kuanzisha mchakato mpya wa kanuni maadili, usiotaka kumshirikisha
Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wa maisha; wanataka kumnyamazisha Mungu
kutoka katika undani wa dhamiri zao.
Kardinali Jaime Ortega Alamino anakazia
kwamba, katika mazingira kama haya, kuna haja kwa waamini kusimama kidete kuiungama
Imani ambayo inarutubishwa kwa akili, vinginevyo, imani hiyo inaweza kugeukwa kuwa
ni vionjo na hali ya mtu kujisikia; matokeo yake ni imani kupoteza dira na mwelekeo
na kuanza kuwa ni chanzo cha kero na vurugu ndani ya Jamii, kama inavyojionesha katika
baadhi ya makundi ya waamini wa dini mbali mbali duniani. Hii ni imani inayounda makundi
ya waamini wenye siasa kali, wanaosukumwa na vionjo zaidi kuliko kutumia akili zao
barabara.
Nchini Cuba, Wakristo, wamenyanyasika, wakadhulumiwa na kunyamazishwa;
mambo ambayo yanawafanya wananchi hao hadi leo hii, kuendelea kuishi katika hali ya
wasi wasi na kuchanganyikiwa. Imani yao kwa Kristo iwajengee uwezo wa kukutana na
Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Ni mwaliko wa kushiriki kikamilifu
katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato mzima wa kuyatakatifuza malimwengu;
kila mwamini akijitahidi kuchangia katika ujenzi wa Jamii, ili kupata mahali pazuri
zaidi pa kuishi.
Ili kufanikisha azma hii, hakuna haja ya kufanya ugunduzi
mkubwa wa kisayansi wala kwenda kuvinjari angani kwa ajili ya kutosheleza vionjo na
hisia za mwanadamu, bali ukuaji na ukomavu wa maisha ya kiroho; unaothubutu kubainisha
maana ya maisha, kwa kujikita kutafuta na kudumisha misingi ya haki na matumaini kwa
wale waliokata tamaa ya maisha. Anawaalika Wakristo nchini Cuba kujibidisha katika
azma ya Uinjilishaji Mpya, changamoto inayotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Waamini
daima wajitahidi kufanya rejea ya Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni Imani
ambayo mara nyingi, haikueleweka, imefutwa katika historia ya familia na watu wengi
kutokana na kumezwa mno na malimwengu; kwa kutangaza tanga katika madhehebu mbali
mbali ya Kikristo; kwa kuwa na misimamo mikali ya kiimani bila kusahau mifano mibaya
ambayo imetolewa hata na Wakristo wengine.
Kardinali Jaime Ortega Alamino
anasema, mtu akibahatika kukutana na Yesu katika hija ya maisha yake, kwa hakika,
huyo atabadilika tu! Ni mtu ambaye atafanikiwa kuwa na mwelekeo na mawazo mapya, atakuwa
na kukomaa, tayari kushuhudia mshikamano huo na Kristo pamoja na Kanisa lake.