2012-11-23 14:08:38

Falme za Kiarabu kuzindua Kituo cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni cha Kimataifa mjini Vienna


Kituo cha Kimataifa cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni cha Mfalme Abdullah Bin Adbulazizi, kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mjini Vienna hapo tarehe 26 Novemba 2012. Hizi ni juhudi za pamoja kati ya Falme za Kiarabu, Austria na Ufalme wa Hispania na Vatican inashiriki kama nchi mtazamaji. Katika tukio hili, Vatican itawakilishwa barabara.

Hayo yamesemwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, lengo la taasisi hii ni kukuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni; ili watu waweze kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao, hatimaye, waweze kuishi kwa amani na utulivu, kwa leo na kesho yenye matumaini zaidi.

Itakumbukwa kwamba, haya ni matunda ya mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita na Mfalme Abdullah Bin Abdulaziz, yaliyofanyika tarehe 6 Novemba 2007 hapa mjini Vatican. Kimsingi ni mali ya Falme za Kiarabu, inayojitegemea pamoja na kuwa na utambulisho wa kimataifa mintarafu Umoja wa Mataifa.

Hapa ni mahali ambapo panaweza kutumika kwa ajili ya majadiliano ya kidini na kitamaduni, kwa vile Vatican ina utajiri mkubwa katika mada hii, uwepo wake ni jambo muhimu pamoja na kuheshimu asili yake. Anasema, Padre Federico Lombardi.







All the contents on this site are copyrighted ©.