2012-11-22 08:30:43

Waislam na Wakristo wanapaswa kushirikiana na kushikamana ili kudumisha haki ndani ya Jamii


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kiislam ya Majadiliano ya Kidini, kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2012 walifanya mkutano wa nane uliokuwa unajadili kuhusu ushirikiano kati ya Waislam na Wakatoliki katika kudumisha amani ulimwenguni.

Mada hii iligawanywa tena katika vipengele vilivyojadili kuhusu: dhana ya haki, haki mintarafu maisha ya mwanadamu, haki katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii pamoja na kuangalia haki kwa ajili ya Familia ya binadamu.

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu uliokuwa unafanyika hapa mjini Vatican uliongozwa na Kardinali Jean Lous Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini na upande wa Taasisi ya Kiislam ya Majadiliano ya kidini, ujumbe wake uliongozwa na Dr Mohammad Bagher Korramshad, Rais wa Taasisi hii.

Katika tamko lao la pamoja, wajumbe wanasema kwamba, mkutano huu umefanyika katika hali ya kirafiki, jambo lililowawezesha wajumbe kushirikishana mawazo kuhusiana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo: hasa zaidi: athari za myumbo wa uchumi kimataifa, utunzaji bora wa mazingira, sera zinazoendelea kudhohofisha misingi ya maisha na familia bora pamoja na vitisho dhidi ya amani duniani.

Wajumbe wanatambua tofauti zao za kidini, lakini wanafahamu fika kwamba, kuna mambo ambayo yanawaunganisha kwa pamoja nayo ni: Imani katika Mungu mmoja, Muumbaji anayetoa fursa ya kufahamu misingi ya haki inayoweza kutekelezwa katika ngazi ya mtu binafsi, Jumuiya; katika maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimahakama.

Haki ni fadhila inayojikita katika utu na heshima ya binadamu inayohitaji matumizi sahihi ya akili inayoangaziwa na Mwenyezi Mungu. Kila mtu anawajibu wa kutambua na kuheshimu uhuru wa dhamiri, kwani hii ni misingi thabiti inayopania kudumisha haki ndani ya Jamii. Uelewa makini wa dhana ya haki, inawasaidia waamini wa dini hizi kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Ni wajibu wa kimaadili kwa viongozi kupinga aina zote za ukiukwaji wa haki na kwamba, wanachangamotishwa kusimama kidete kukuza na kuendeleza haki sehemu mbali mbali za dunia. Viongozi hawa wa kidini wanabainisha kwamba, wanazo nyenzo za kutosha, zinazoweza kutumika ili kutekeleza misingi ya haki na amani katika uhalisia wake. Waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kuendelea kufahamiana na kushikamana kwa karibu zaidi ili kukuza majadiliano ya kidini na ushirikiano.

Wajumbe kwa pamoja wameahidi kuhakikisha kuwa matunda ya mkutano huu yanatangazwa kwa waamini wa Jumuiya na Jamii wanamoishi, ili kuleta mabadiliko duniani. Wanamshukuru kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyewapokea na kuzungumza nao mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 21 Novemba 2012. Mkutano mwingine unatarajiwa kufanyika nchini Tehran, katika kipindi cha miaka miwili ijayo, lakini utatanguliwa na kamati ya maandalizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.