2012-11-22 10:16:19

Tanzania inapania kupata Katiba Mpya na nchi kuendelea kuwa na amani na umoja wa kitaifa!


Rais Jakaya Kikwete Jumatano tarehe 21 Novemba, 2012 katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon, zilizowasilishwa na Bw. Serge Mickoto. Katika salamu hizo, Rais Bongo amemtaka Rais Kikwete kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali.

Rais Kikwete amemwambia mjumbe huyo wa Rais Bongo, kuwa Tanzania inathamini ushirikiano uliopo na juhudi za kuuendeleza ushirikiano huu ni muhimu kwa nchi zote mbili.

Mapema asubuhi Rais Kikwete amepokea hati za utambulisho za mabalozi kutoka Iran na Canada. Wa kwanza kuwasilisha hati zake ni balozi Mehdi Agha Jafari na kufuatiwa na Balozi wa Canada Bw. Alexandre Leveque. Mara baada ya kupokea hati zao Rais Kikwete amefanya mazungumzo na Mabalozi hao na kuwaeleza hali ya kisiasa na ushirikiano baina ya nchi zao na Tanzania.

Rais amemueleza Balozi wa Canada kuhusu mchakato wa Katiba unaoendelea nchini sasa hivi na kumueleza kuwa anatarajia kuwa nchi itapata Katiba itakayohakikisha nchi inabakia kuwa na Amani na Umoja. “Tunataka kuhakikisha kuwa Umoja wa Kitaifa unabakia, hakuna migawanyiko ya kidini wala kikabila, tunataka Katiba ambayo haitaleta migawanyiko ya aina yeyote wala kupendelea kundi lolote nchini Mwetu” Rais amesisitiza.









All the contents on this site are copyrighted ©.