Mikakati ya maboresho ya maisha na hali ya kazi ya mabaharia duniani; uharamia na
changamoto zake!
Wajumbe wa Kongamano la ishirini na tatu juu ya Utume wa Bahari, lililoandaliwa na
Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum hapa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 22 Novemba, 2012, wanaendelea
kuchambua madhara yanayosababishwa na maharamia baharini pamoja na hali ya maisha
ya mabaharia na familia zao wanaokumbana na mikasa kama hii.
Vitendo vya uharamia
vimeongezeka kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni hasa katika mwambao wa Bahari
ya Hindi, na kwenye nchi zinazounda Pembe ya Afrika. Usalama wa maisha ya mabaharia
na mali wanazobeba uko mashakani, hali inayopelekea pia kuongezeka kwa gharama za
usafirishaji.
Itakumbukwa kwamba, Kongamano hili kwa namna ya pekee, linapania
kukoleza juhudi za Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa mabaharia kwani Habari Njema
ya Wokovu inapasa kumgusa kila mtu mahali alipo na katika utume wake, kama alivyobainisha
Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya, wakati
akichangia mada juu ya Uinjilishaji Mpya katika Ulimwengu wa Mabaharia.
Shirika
la Kazi Duniani, ILO baada ya kazi kubwa ya miaka saba, hatimaye, kuanzia mwaka 2013
kutakuwa na chombo madhubuti kinachopania kuboresha maisha na hali ya kazi kwa mabaharia
zaidi ya millioni moja na laki mbili, wanaotekeleza kazi yao sehemu mbali mbali za
dunia.
Serikali zitapaswa kuhakikisha kwamba, katika bandari zao kuna msaada
wa kisheria, utakaorahisisha mabaharia kupata huduma za kijamii, matibabu, chakula,
mahali pa kufanyia michezo pamoja na fursa ya kuwasiliana na familia zao. Mabaharia
pia watapatiwa fursa ya kushiriki katika maisha ya kiroho ya dini zao wanapokuwa bandarini.
Wajumbe
wa kongamano hili wanasema kwamba, uharamia kwa sasa ni tatizo nyeti, linaloendelea
kukuza na kupanuka kwa kasi kubwa hasa kwenye Bahari ya Hindi, ingawa uharamia huu
unafanyika kwa malengo na mifumo mbali mbali. Baadhi ya wajumbe, wametoa ushuhuda
wa jinsi ambavyo kwa miaka mingi wamekuwa wakijihusisha na majadiliano kati ya mabaharia
na maharamia; majadiliano ambayo yamewezesha Mabaharia na meli zao kuachiwa huru ili
kuendelea na safari zao.
Mabaharia wakati mwingine wanashikiliwa mateka kwa
kipindi kirefu, hali ambayo inasababisha usumbufu mkubwa, baadhi ya mabaharia waliotekwa
wanashuhudia kwamba, kipindi chote hiki kwao imekuwa ni Njia ya Msalaba, wamekitumia
kwa ajili ya kusali zaidi, kwani daima waliyaona maisha yao kuwa hatarini.
Wajumbe
wamezungumzia pia dhamana na nafasi ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwa mabaharia,
kama utume wa Mama Kanisa kwa mabaharia ili kukidhi kiu ya maisha yao ya kiroho. Huu
ni ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Mama Kanisa tangu Mwaka 1930 amekuwa bega kwa
bega na mabaharia katika safari zao baharini, daima akiwaonesha dira ya matumaini
katika furaha, shida na mahangaiko yao ya ndani. Meli za abiria ni jukwaa linaloweza
kutumiwa na Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya.