Magereza iwe ni shule ya mafunzo endelevu na fursa ya kuonja ushindi wa Kristo kwa
njia ya Fumbo la Pasaka dhidi ya dhambi na uovu!
Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kusababisha matabaka ya kijamii na
ubinafsi mambo ambayo yanachochea kwa kiasi kikubwa tabia ya makosa ya jinai, mada
ambayo inapaswa kujadiliwa katika mapana yake si kwa kuwaachia tu watunga sheria,
bali kuangalia pia jinsi ambavyo sheria inatekelezwa katika utoaji wa adhabu.
Haki
inapaswa kuzingatia na kuheshimu utu na haki msingi za binadamu, mambo ambayo bado
hayatekelezwa kikamilifu katika nchi nyingi duniani, kwani haki msingi za mtu binafsi
zinaendelea kuvunjwa mara kwa mara, changamoto ya kuwa na mwelekeo mpya ili magereza
yawe kweli ni mahali pa kurekebisha tabia, ili mfungwa anapomaliza adhabu yake, aweze
kupokelewa tena katika Jamii, huku akionesha ukomavu na kwamba, sasa yuko tayari kutafuta
mafao ya wengi ndani ya Jamii.
Ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, kwa wajumbe wa mkutano wa kumi na saba wa Viongozi wakuu wa magereza
Ulaya, walipokutana naye Alhamisi, tarehe 22 Novemba 2012 mjini Vatican. Anasema,
katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya wafungwa,
lakini bado kuna njia ndefu inayopaswa kufuatwa. Hapa si suala la fedha, bali ni pamoja
na kuhakikisha kwamba, wafungwa wanaishi katika mazingira bora yanayoheshimu na kuthamini
utu wao kama sehemu ya majiundo ya wafungwa.
Kuna umuhimu wa kubadili mawazo,
ili kuheshimu na kuthamini haki msingi za wafungwa na jinsi ya kutekeleza adhabu kutokana
na makosa waliyotenda. Lengo la adhabu liwe ni kumwelimisha mfungwa, ili aweze kutenda
haki; wasaidiwe kuwa ni watu wema wanapokuwa wanatumikia vifungo vyao, kwa kuhakikisha
kwamba, wanatendewa haki. Inasikitisha kuona kwamba, magereza badala ya kusaidia kubadili
tabia na mwenendo wa wafungwa, yanachochea ukatili na uvunjifu wa sheria.
Baba
Mtakatifu anawakumbusha wakuu wa magereza kwamba, wanaweza kutekeleza wajibu wa kusimamia
haki kwa kuwamegea wengine upendo unaojishikamanisha na utu wa mwanadamu. Ni viongozi
ambao wamekabidhiwa dhamana inayowataka kuwa makini sana, kwani kazi yao ni nyeti,
kwani inamgusa mtu aliyekosa, anayetekeleza adhabu ya makosa yake, lakini anahitaji
pia kuheshimiwa na kuthaminiwa kama binadamu, bila kudhalilishwa wala kubezwa.
Huu
ndio utume uliotekelezwa na Yesu kwa kutambua kwamba, wadhambi walikuwa ni watu ambao
walikuwa na nafasi kubwa ya kupokea huruma ya Mungu katika maisha yao na kwamba, kila
mtu anaalikwa kuwa ni mwangalizi wa ndugu yake. Kama wakuu wa magereza, wanapewa dhamana
ya kuwatunza wafungwa, ambao wanakabiliwa na hatari kubwa ya kutokutambua maana ya
maisha, utu na heshima yao, matokeo yake ni kukata tamaa.
Kuna haja kwa Jamii
kuwaheshimu wafungwa na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya majiundo yao makini,
ili magereza yageuke na kuwa ni Jumuiya inayoelimisha. Wafungwa kutoka nchi za nje
ni jambo ambalo linaendelea kusababisha ugumu na kuwa ni hatari zaidi.
Wafungwa
wanapaswa kuonesha utashi wa kufanya mabadiliko na mageuzi katika maisha yao, kwa
kushiriki kikamilifu katika mikakati inayotolewa kwa ajili ya lengo hili. Wafungwa
wapewe pia huduma za maisha ya kiroho, kwa kutambua kwamba, ndani mwao wanayo chapa
ya sura na mfano wa Mungu ambayo kamwe haiwezi kufutika hata wanapokuwa gerezani.
Ni
matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwamba, magereza yatakuwa kweli
ni mahali pa mafunzo endelevu na fursa ya kuonja ushindi wa kazi ya ukombozi iliyofanywa
na Kristo kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa Fumbo
la Pasaka akaonesha ushindi dhidi ya uovu na nguvu za giza.