2012-11-22 10:28:26

Kituo cha kulelea Watoto Wenye Ulemavu wa Akili, cha Miyuji Cheshier cha Sherehekea Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake!


Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mutinda Mutiso amesema kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyojenga barabara nyingi za lami zenye ubora katika maeneo mbalimbali ya nchini humo. Balozi Mutinda Mutiso ametoa kauli hiyo Jumatano tarehe 21 Novemba 2012, katika hafla ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa kituo cha kulelea Watoto Wenye Ulemavu wa Akili cha Miyuji Cheshier Home.

Akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa Serikali ya Tanzania imejitahidi sana kujenga miundombinu ya barabara za lami katika mikoa mingi tofauti na nchi nyingine jambo ambalo linaharakisha maendeleo. Ametolea mfano nchi ya Kenya ambayo ni ndogo sawa na mara mbili kwa Tanzania, lakini, miundombinu ya barabara nchini Tanzania inaendelea kuboreshwa.

Aidha amesisitiza amani hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania ipo katika mchakato wa kuunda katiba mpya ambayo itakamilika kabla ya mwaka 2015. Amewaasa wakazi wa Dodoma kujenga utaratibu wa kukisaidia kituo hicho cha watoto wenye ulemavu wa akili, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, kadiri ya uwezo wao.

Balozi Mutiso ametoa msaada wa vyakula na fedha zaidi ya shilingi milioni moja ili kusaidia kituo hicho, Aidha amekabidhi dola za kimarekani zaidi ya mia tatu kwa Masista wa kituo hicho na wote wanaowalea watoto hao.

Awali akizungumza wakati wa Ibada ya Misa takatifu, Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, alisisitiza upendo kwa jamii na hasa kusaidia makundi ya wasiojiweza ili nao waweze kujikimu. Askofu Nyaisonga ameeleza kuwa yapo makundi ambayo hayana mtu wa kuwasaidia isipokuwa Mungu hivyo, Mungu hutumia wanadamu kusaidia makundi hayo.

Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili cha Miyuji Cheshire, kilianzishwa na Askofu mstaafu Mathias Joseph Issuja wa Jimbo Katoliki Dodoma, baada ya kuguswa na matatizo na changamoto zilizokuwa zinawakabili watoto wenye ulemavu wa akili kwenye familia zao. Kituo hiki kimekuwa ni alama ya matumaini na mshikamano wa upendo unaopania kuenzi utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu








All the contents on this site are copyrighted ©.