2012-11-21 08:24:17

Serikali na wananchi wa Kenya; komesheni vurugu zinazoweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeitaka Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba, wanakomesha vitendo vya vurugu na ghasia ambayo vimeendelea kutawala maeneo kadhaa nchini Kenya katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema inasikitisha kuona kwamba, mbegu ya chuki, uhasama na kulipizana kisasi inaendelea kupanuka siku hadi siku, kiasi cha kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu.

Mauaji ya askari arobaini pamoja na raia kumi ni matukio ya kusikitisha sana na kwamba, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa majadiliano na upatanaisho kati ya makabila nchini Kenya, ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, badala ya mwelekeo wa sasa unaotaka kuligawa taifa katika makundi ya kikabila na kimajimbo. Wakenya pia wanapaswa kuwa makini na choko choko za kidini zinazoendelea chini kwa chini, kwani zinaweza kuwa ni chanzo kikuu cha maafa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, limetuma salam zake za rambi rambi kwa wote walioguswa na misiba ya kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao katika vurugu zilizotokea hivi karibuni nchini Kenya. Serikali na wananchi kwa ujumla wanapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, vinginevyo, hata uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani, unaweza kuwa mashakani.

Wananchi wapewe elimu ya uraia pamoja na kuendelea kushuhudia umuhimu wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthaminiana miongoni mwa watu wa dini, madhehebu na makabila tofauti, wakitambua kwamba, wote wanaunda nchi moja ya Kenya. Upatanisho wa kitaifa ni hoja ya nguvu inayopaswa kufanyiwa kazi na wananchi wote wa Kenya kwa ajili ya mustakabali wa nchi yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.