SECAM yaanza semina kuhusu imani, utamaduni na maendeleo Jijini Dar Es Salaam
Baraza ka Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, wanaendelea na semina inayojadili kuhusu imani,
utamaduni na maendeleo. Semina hii imefunguliwa rasmi hapo tarehe 20 Novemba na inatarajiwa
kuhitimishwa tarehe 24 Novemba 2012 na inawashirikisha wawakilishi sabini kutoka katika
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar.
Mada zinazojadiliwa kwa
sasa ni pmoja na umuhimu wa kuwa na miundo mbinu itakayosaidia mchakato wa majadiliano
kati ya Kanisa Barani Afrika na tamaduni na maendeleo endelevu kwa kuwashirikisha
viongozi wa Kanisa, wanataalimungu, waamini na Waafrika ambao wanaishi uhamishoni.
Lengo ni kuendeleza dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji sanjari na utamadunisho
kwa kuangalia fursa, changamoto na matarajio kwa siku za usoni.
Wajumbe wanapembua
kwa kina na mapana kuhusu utamaduni wa Mwafrika na Maendeleo endelevu barani Afrika
wakati wa utandawazi; umuhimu wa kujenga na kuimarisha utawala bora pamoja na sera
za Afrika kuhusu maendeleo. Ni siasa zipi ambazo zinafumbatwa katika kuchanganua mikakati
ya maendeleo Barani Afrika.
Ni wakati kwa nchi wanachama wa SECAM kuanzisha
jukwaa la imani, utamaduni na maendeleo, kama sehemu ya utekelezaji wa Nyaraka za
Kichungaji: Kanisa Barani Afrika na Dhamana ya Afrika zilizotolewa na Kanisa baada
ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu Barani Afrika.
Semina hii inachukuliwa
kama fursa muhimu kwa Kanisa Barani Afrika kama Familia ya Mungu inayopania kuendeleza
mchakato wa kukusanya na kuunganisha mambo yatakayosaidia kukuza na kuimarisha imani,
utamaduni na jukwaa na maendeleo Barani Afrika.
Semina hii imetanguliwa na
Kikao cha Kamati tendaji ya SECAM chini ya uongozi wa Kardinali Polycarp Pengo, Rais
wa SECAM. Kamati tendaji imejadili pamoja na mambo mengine sera na mikakati inayopaswa
kufanyiwa kazi kwa wakati huu pamoja na kufanya tathmini ya mradi wa utawala bora
unaoendeshwa na SECAM kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu
Katoliki Ujerumani, Misereor, mradi ambao ulizinduliwa tangu mwaka 2006.