2012-11-21 07:38:08

Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni vyombo madhubuti vya kurithisha Imani ya Kikristo


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena katika idhaa yetu ya Kiswahili. Hewani ni kipindi chetu cha uinjilishaji wa kina ambapo tunaendela bado kuchambua hati ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni hapa Vatican. RealAudioMP3

Juma hili karibu tuchambue neno la Mungu, uenezaji wa Imani, mawakala wa uinjilishaji, maisha ya ushuhuda na matunda ya uinjilishaji mpya.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anaanza kwa kubainisha kuwa tangu Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, Kanisa Katoliki limegundua kuwa uenezaji wa Imani ni makutano ya ana kwa ana na Kristu mwenyewe kupitia Neno lake na Mapokeo ya Kanisa kwa maongozi na msaada wa Roho Mtakatifu. Kila kizazi na kila zama zimeendelea kukutana na Kristo katika Imani Katoliki kwa njia ile ile na hivi Kanisa linaendelea kuwa hai likitimiza utume wake lililokabidhiwa na Kristo Mwenyewe licha ya changamoto mbali mbali za mabadiliko ya nyakati na mazingira.

Ekaristi Takatifu imebaki daima kuwa kiungo cha mapendo kinachowaunganisha wanafamilia ya Mungu kutoka pande zote za dunia kwa kuumega mkate mmoja katika Kristo na hivi kuwa mwili mmoja na Roho moja.

Hivyo Baba Mtakatifu amelitaka Kanisa kutafakari kwa makini namna litakavyojizatiti kutangaza Neno la Mungu kwa vizazi vijavyo. Mazingira yanaonesha kwamba kuna hamu na hamasa miongoni mwa vijana kulisikia Neno la Mungu na kumjua Yesu. Hivyo kuna haja kwa Kanisa kujifunga kibwebwe na kujitoa kimaso maso kuliweka wazi Neno hili mbele ya vijana.

Kuna haja ya kuwasaidia vijana kujipa moyo na kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu bila kuogopa ili kwa Neno hilo wakapate kutambua nafasi yao katika ulimwengu huu na katika Kanisa na hivyo kukua kiimaadili na uchaji wa Mungu. Lakini vijana wanahitaji ushuhuda wa Neno la Mungu na maisha ya Imani hai kutoka kwa Kanisa yaani wazazi, jumuiya na wachungaji. Makundi haya lazima yajipange kuwa na vijana ili wajinze kutoka ushuhuda wao.

Kufanikisha hilo Baba Mtakatifu Benedikto XVI amesisitiza umuhimu wa Katekesi ya Kina. Vijana wapewe mafundisho msingi ya Imani wakati wa maandalizi kupokea masakramenti, lakini pia katika ngazi mbali mbali Katekesi iendelee katika vikundi vya vijana hata baada ya kupokea masakaramenti. Kwa maneno mengine kuwepo kwa Katekesi endelevu katika marika yote ya jamii.

Sambamba na hili waalimu wa Katekesi waandaliwe vizuri ili waweze kutoa majibu kwa maswali mengi ya vijana kuhusu mambo ya Imani. Kazi hii pengine wasiachiwe Maketekista tu bali kila mmoja na hasa Mapadre na Watawa wahusike moja kwa moja katika mafundisho ya Katekesi. Baba Mtakatifu Benedikto XVI ni mfano halisi wa Walimu wa Katekesi kwa wale wanaosikiliza mafundisho yake ya kila Jumatano katika Basilika la Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu ameyataja Makanisa mahalia kuwa wakala wakuu wa utangazaji, uenezaji na mashahidi wa imani katika Kanisa. Kwa msingi huo Kanisa zima linahusika katika utume huu wa kimissionari. Baba Mtakatifu amenukuu mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican kuwa Roho Mtakatifu huwakusanya waumini katika vikundi ambavyo huishuhudia imani ambayo hujionesha katika kulisikiliza Neno la Mungu, kushirikishana mang’amuzi kadiri kila mmoja anavyoangaziwa na Roho, kusaidiana kidugu na kuuishi upendo wa Mungu kama unavyoainishwa na Kristu mwenyewe.

Kumbe, kuna haja ya kuimarisha jumuiya ndogondogo na vikundi mbali mbali katika Kanisa kwa madhumuni haya ya uinjilishaji. Vikundi hivi ni uwepo halisi wa Kanisa vikiungana na Wachungaji wake ndani ya Kanisa.

Kulingana na mazingira yaliyopo Makanisa mahalia yanaalikwa kuwajibika na kuhusika moja kwa moja na uinjilishaji kwa kujiaminisha kabisa kwa Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa daima kiasi kwamba makanisa haya yaweze kwa nguvu, kasi na ari mpya kuendeleza utume wa Kanisa. Wakristu katika ujumla wao wajisikie kutoka ndani kuhusika kuitikia wito wa Kristo wa kumtangaza kwa mataifa yote kila mmoja kwa maisha yake aliyoitiwa: kama mwanafamilia, katika fani mbali mbali, maisha ya wakfu n.k.

Mpendwa msikilizaji, wakati ukuta. Hadi hapa, tumefikia mwisho wa uchambuzi wetu kwa juma hili. Naomba nikuage nikikutakia kila heri na baraka kutoka kwa Mungu. Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.









All the contents on this site are copyrighted ©.