Fungueni akili zenu kwa mwanga wa ukweli wa Mungu unaoonesha utukufu wa utu na wito
wa mwanadamu
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wakati
wa Katekesi yake, Jumatano 21 Novemba, 2012, ameendelea kuwahimiza waamini kutambua
maana ya imani, kama njia ya kukutana na mng'ao wa ukweli wa Mungu.
Kwa njia
ya imani, mwamini anapata ufahamu kumhusu Mungu, yeye mwenyewe na kujifunza kuishi
kwa busara katika ulimwengu huku akingojea utimilifu wa maisha na furaha ya uzima
wa milele ujao. Imani na akili anasema Baba Mtakatifu ni mambo yanayofanya kazi kwa
pamoja ili kufungua akili ya mwanadamu kuhusu ukweli wa Mungu. Kwa asili imani inapania
kuelewa, wakati ambapo akili inatafuta ukweli, mwongozo na utimilifu wake kwa njia
ya kukutana na Neno la Mungu ambalo limefunuliwa kwake.
Baba Mtakatifu anakazia
kwamba, kimsingi hakuna msigano kati ya imani na sayansi, kwani yote yanapania kumhudumia
mwanadamu katika maisha yake ya kimaadili na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. Habari
Njema ya Wokovu kuhusu Yesu Mwana wa Mungu, inaonesha ubinadamu ambao ni muhimu sana
katika kulielewa Fumbo la Mwanadamu na Ulimwengu. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawawezeshe
waamini kufungua akili zao kwa mwanga wa ukweli wa Mungu, unaoonesha utukufu wa utu
na wito wa mwanadamu.
Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wajumbe wanaoshiriki
katika mkutano wa ushirikiano kati ya waamini wa Kanisa Katoliki na waaminiwa dini
ya Kiislam, katika mchakato unaopania kudumisha haki katika ulimwengu mamboleo. Amewashukuru
wanachama wa Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, CAFOD linaloadhimisha
Jubilee ya miaka hamsini tangu lililopoanzishwa, kielelezo cha mshikamano wa upendo
na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu
anasema, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, inayoadhimishwa na Mama Kanisa
kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba, iwe ni kielelezo na mfano wa kuigwa kwa kujitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu sanjari na kutekeleza mapenzi yake. Mama Kanisa
pia anaadhimisha Siku ya Watawa wa ndani, walioitwa kumfuasa Kristo kwa njia ya taamuli.
Anapenda kuwahakikishia uwepo wake na ule wa Kanisa zima.
Anawaalika waamini
na watu wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwuwa, wanawasaidia watawa wa ndani kwa hali
na mali, kwani wao ni msaada mkubwa kwani wamewekwa wakfu kwa ajili ya kuliombea Kanisa
na Ulimwengu kwa ujumla.
Kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Makanisa makuu ya
Mtakatifu Petro na Paulo yaliyoko hapa mjini Roma, hivi karibuni, iwe ni chachu ya
kukuza na kuimarisha upendo wao kwa Kanisa lililojengwa juu ya msingi wa maisha ya
Mitume.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewakumbusha waamini kwamba,
Jumapili ijayo, Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, mwaliko
kwa waamini kumweka Kristo kuwa ni kiini cha maisha yao, ili waweze kujichotea mwanga
na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha ya kila siku.
Kwa wagonjwa
na wote wanaoteseka, Msalaba wa Kristo uwe ni faraja na kielelezo cha mshikamano wa
dhati na wanandoa wapya wanahimizwa kutambua uwepo wa Kristo kati yao na wanapoendelea
na hija ya maisha ya ndoa, katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa
katika upendo na amani.