Kongamano la ishirini na saba kimataifa juu ya Utume wa Bahari, linaendelea kujadili
kuhusu mchakato wa maboresho ya maisha ya mabaharia kwa kuwahakikishia huduma bora
pamoja na kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho.
Haya ni kati ya malengo yanayofanyiwa
kazi na Utume wa Bahari, kwa kuungana na Shirikisho la Wasafirishaji Kimataifa linalounganisha
vyama vya wafanyakazi mia saba na nane, ili kuwawakilisha wafanyakazi zaidi ya millioni
tano, wanaohudumia takribani nusu ya usafiri wa bahari duniani.
Kongamano
hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu
wasiokuwa na makazi maalum, wakiongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu
wa mabaharia: nyenzo na mbinu mpya za kutangaza Habari Njema ya Wokovu." Wajumbe wanaendelea
kutoa ushuhuda wa maisha yao binafsi jinsi ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia
na kuwwahudumia mabaharia sehemu mbali mbali za dunia.
Utume wa Bahari unawashirikisha
watu wa dini na madhehebu mbali mbali, wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya
maendeleo na ustawi wa mabaharia, kama ilivyojionesha kwa Mama Apinya Tajit, anayetekeleza
utume wake kwenye Bandari za Thailand. Yeye anasema, anakutana zaidi na waamini wa
dini ya Kiislam ambao wanafanya kazi baharini.
Kundi kubwa la mabaharia hawa
wanajikuta wakati mwingine hawana chakula, wananyanyasika na kudhulumiwa haki zao
msingi; wanatekwa na wakati mwingine wanakumbana na uharamia ambao kwa sasa umekuwa
ni tishio kubwa katika usafiri wa bahari. Wao wanatoa huduma ya ushauri nasaha pamoja
na kuhakikisha kwamba, walau wanapata mahitaji yao msingi kwa wakati huo.
Mradi
wa ustawi wa jamii kwa ajili ya mabaharia nchini Italia, ni ushuhuda unaonesha kwamba,
bandari zinaweza kugeuzwa kuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha urafiki na mahusiano
mema. Kutokana na sababu za kiusalama, mabaharia wanapotua nanga hawaruhusiwi kushuka
katika Meli zao kwa muda mrefu kutokana na hofu kwamba, wanaweza kutelekeza Meli zao
na kuishia mitaani kutokana na sababu mbali mbali wanazokabiliana nazo.
Imetokea
pia kwamba, kuna Meli zimeachwa bandarini na mabaharia kukosa mshahara, chakula na
maji, kiasi hata cha kushindwa kurudi nyumbani kwao! Mtandao wa Utume wa Bahari umekuwa
mstari wa mbele kuwasaidia Mabaharia hawa katika shida na mahangaiko yao, jambo ambalo
kwa hakika, limejenga utamaduni wa upendo na mshikamano.
Kimsingi, mabaharia
wanakabiliana na hali ngumu ya maisha wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, lengo
la Utume wa Bahari ni kushiriki katika maboresho ya maisha ya wafanyakazi hawa, kwa
kutambua na kuthamini utu na heshima yao, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki
zao msingi; huku wakikazia ubora wa vyombo vinavyotumika.
Tarehe 21 Novemba
2012, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wavuvi Duniani, fursa nzuri kwa ajili
ya kuwakumbuka wavuvi kutokana na changamoto zinazowasibu katika maisha yao! Hatari
na mazingira magumu wanayokumbana nayo, ili kuhakikisha kwamba, walau watu wengi wanapata
kitoweo cha samaki mezani. Ni kundi linalo nyanyasika na kudhulimiwa, linalohitaji
kutetewa kadiri ya sheria za kimataifa, ili hatimaye, kukidhi mahitaji ya mabaharia
sehemu mbali mbali za dunia.