2012-11-20 09:53:04

Siku ya Watoto Wote Duniani, 20 Novemba 2012


Mheshimiwa Padre Pascual Chàves Villanueva, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco, anasema, anachukua fursa hii kuungana na viongozi mbali mbali wa kidini katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Wote Duniani, inayoadhimishwa tangu mwaka 2009, tarehe 20 Novemba ya kila mwaka, kushirikiana kwa vitendo ili kulinda na kutetea haki za watoto ambao bado hawajaandikishwa walipozaliwa.

Maadhimisho ya Siku ya Watoto Wote Duniani ni changamoto kwa viongozi wa kidini kutaka kuunganisha nguvu zao, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee, kwa mwaka 2012, Padre Pascual Chàves anapenda kuwaalika Wasalesiani pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuungana nao katika kusali ili kufanikisha jitihada za uandikishaji wa watoto wanapozaliwa, kama nyenzo muhimu ya kupambana na baa la umaskini na nyanyaso. Lengo ni kuhakikisha kwamba, hakuna tena mtoto ambaye hatambulikani kwa vile tu hakuweza kuandikishwa siku ile alipozaliwa kutokana na sababu mbali mbali.

Inakadiriwa kwamba, kuna jumla ya watoto zaidi ya millioni hamsini kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao hawatambuliwi kwa sababu hawajawahi kuandikishwa na matokeo yake, wanakosa fursa za elimu, afya na wakati mwingine wanajikuta wakitumbukizwa katika biashara haramu ya watoto.

Kati yao wanaishi katika mazingira hatarishi, wanafanyishwa kazi za suluba au hata kuolewa katika umri mdogo. Cheti cha kuzaliwa kinampatia mtoto haki zake msingi, zinazopaswa kulindwa na kuheshimiwa. Bila ya cheti hiki, watoto hawa watajikuta wakinyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi.

Mkuu wa Shirika la Wasalesiani anatambua kwamba, Familia ya Wasalesiani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, inawahudumia vijana zaidi ya millioni kumi na tano, huu ni urithi ambao wanauthamini, wakati huu, Shirika lake linapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka mia mbili tangu Mtakatifu Yohane Bosco, Baba na Mwalimu alipozaliwa. Wasalesiani pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, waunganishe nguvu zao kwa ajili ya ukombozi wa watoto sehemu mbali mbali za dunia; kwa kulinda haki zao msingi na bila ubaguzi wowote ule.







All the contents on this site are copyrighted ©.