2012-11-20 08:20:44

Maaskofu wa Caritas Afrika wanakutana Kinshasa, DRC. kujadili utambulisho wa Caritas Barani Afrika


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, kwa kushirikiana na Maaskofu wa Afrika wanaosimamia na kuratibu Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika, Caritas, kuanzia tarehe 20 Novemba hadi 22 Novemba 2012 wako Kinshasa, DRC kujadili kuhusu utambulisho wa Kanisa Katoliki Barani Afrika, mintarafu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Mungu ni Upendo, Deus Caritas est!

Hii ni fursa makini kwa Maaskofu wa Afrika kupembua kwa kina na mapana dhamana ya Caritas kama kielelezo cha mshikamano na Makanisa mahalia. Mkutano huu unahudhuriwa pia na Kardinali Oscar Andrès Rodrìguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki.

Utambulisho wa mashirika ya misaada yanayosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki imekuwa ni mada ambayo inafanyiwa kazi na Kanisa katika ujumla wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, Caritas Barani Afrika, limekuwa ni Shirika ambalo liko mstari wa mbele katika kuwahudumia watu wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha hasa zaidi kutokana na umaskini, ujinga na maradhi, matatizo ambayo yakivaliwa njuga na kila mtu akatekeleza wajibu wake ni mambo yanayoweza kutoweka kabisa kama si kupungua kwa kiasi kikubwa Barani Afrika.

Caritas Barani Afrika inapenda kupembua mikakati ya shughuli za kichungaji inayopania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Itakumbukwa kwamba, mada hizi zimekwisha wahi kufanyiwa kazi kunako mwaka 2002, Kigali, Rwanda na 2006 kule Libreville, Congo. Upendo kwa Mungu na jirani ni kiini cha utekelezaji wa majukumu na mipango ya Caritas kadiri ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na viongozi wa Kanisa katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Shirika la Caritas linatekeleza utume wake chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na katika ngazi ya Makanisa mahalia, liko chini ya Maaskofu mahalia. Ni Shirika ambalo linapaswa kutekeleza wajibu wake unaojikita katika kweli za Kiinjili, uelewa wa kitaalimungu, maisha ya kiroho; kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana ya Kanisa zima, inayoihusisha pia Familia ya Mungu.

Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anazima kiu ya upendo kwa jirani yake, hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa njia ya Neno la Mungu na matendo ya huruma. Hiki ni kielelezo cha mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Maaskofu wanatumia fursa hii kuimarisha utambulisho wa Caritas Barani Afrika pamoja na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa Barani Afrika dhidi ya utume na dhamana ya Kanisa.

Caritas inapaswa kuimarisha uhusiano wake na Maaskofu mahalia na kwamba, hili si shirika linalojitegemea bali ni kwa ajili ya maisha na huduma ya Kanisa kwa Familia ya Mungu, kumbe kuna haja ya kutumia vyema rasilimali inayopatikana kwa ajili ya mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.