2012-11-20 11:13:23

Kumfungulia Mungu malango yako ya maisha, si kujiondoa kutoka duniani!


Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliwaandikia ujumbe wa matashi mema, washiriki wa majadiliano na watu wasioamini, yaliyokuwa yanafanyika nchini Ureno, wakiongozwa na kauli mbiu "tunu ya uhai".

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anasema kwamba, kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha ni sehemu ya urithi wa binadamu wote na kwamba, binadamu si tunda la mabadiliko ya kimaumbile, bali kila mwanadamu amenuiwa na kudhamiriwa na Mwenyezi Mungu katika utashi wake.

Anampenda kila mmoja na hivyo anastahili kuishi. Damu azizi ya Kristo inaonesha upendo mkuu wa Mungu na thamani ya binadamu machoni pake na kwa hakika maisha ya mwanadamu yana thamani kubwa sana!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi, mwanadamu anataka kujificha kutoka katika uso wa Mungu, kwa kujiangalia na kujitafuta mwenyewe badala ya kutafuta nguvu za Kimungu, katika ujenzi wa jengo kubwa ambalo halina madirisha; mwanadamu anajukumu la kuhakikisha kwamba, anasaidia kuweka vifaa vya hewa safi na mwanga; lakini hata katika ulimwengu wa namna hiyo, bado mwanadamu anahitaji rasilimali mbali mbali kutoka kwa Mwenyezi Mungu, zitakazotumika kwa ajili ya mafao yake.

Baba Mtakatifu anawaalika wale wasioamini kutambua kwamba, mwanadamu anajukumu la kufungua tena madirisha kwa kuwa na mwelekeo mpya kuhusiana na mbingu na dunia, ili kujifunza kuzitumia vyema. Thamani ya uhai inajionesha kwa namna ya pekee, ikiwa kama mwanadamu anatambua uwepo wa Mungu, changamoto hata kwa wale wasioamini kuishi kana kwamba, kweli Mungu yupo! Inawezekana kuwa hawana nguvu ya kuamini, lakini hata hivyo bado wanaweza kuishi katika nadharia hii.

Kuna matatizo na changamoto mbali mbali duniani, ambazo haziwezi kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, ikiwa kama Mwenyezi mungu hatapewa kipaumbele cha kwanza katika mipango na maisha ya mwanadamu, kwani ni muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha ujumbe wake kwa kusema kwamba, mtu ambaye anajifunua kwa Mwenyezi Mungu bila ya kujiondoka kutoka katika dunia na mwanadamu, bali anamwangalia kila mtu kuwa ni jirani yake; kwa njia ya Mwenyezi mungu ataweza kubomoa kuta za utengano, ili kujenga na kuimarisha umoja na udugu, kwa kutambua kwamba, wote wanategemeana.







All the contents on this site are copyrighted ©.