Kanisa linapania kutangaza Injili ya Upendo kwa vitendo!
Myumbo wa uchumi kimataifa umepelekea kuibuka kwa kundi kubwa la watu wasiokuwa na
fursa za ajira, kumong'onyoka kwa maadili na utu wema pamoja na kuongezeka kwa baa
la umaskini na ujinga duniani, hali inayotishia mustakabali wa familia nyingi.
Askofu Beatus
Kinyaiya wa Jimbo Katoliki Mbulu, katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba,
Kanisa limeendelea kuonesha mshikamano wake wa dhati na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kwa kuwatangazia Injili ya Upendo, inayopania kuwajengea uweze
wa kupambana na hali ngumu ya maisha kwa kuwekeza katika miradi ya elimu, uchumi na
kijamii, dhamana inayotekelezwa kwa namna ya pekee na Shirika la Misaada la Kanisa
Katoliki, Caritas katika ngazi mbali mbali.
Caritas kwa kushirikiana na Wanawake
Wakatoliki Tanzania imeweza kutoa mikopo midogo midogo kwa vijana, wanawake na wakulima
ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kusaidia maboresho ya kilimo chao, ili kiweze
kuwa ni bora na endelevu.
Katika mwelekeo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania lilianzisha Benki ya Mkombozi ili kutoa mikopo kwa wafabiashara na wakulima
ili kuinua hali yao ya kiuchumi na kijamii. Hizi ni jitihada za Mama Kanisa nchini
Tanzania kutangaza Injili ya Upendo kwa vitendo!