Utume wa bahari ni muhimu sana kwa mabaharia, wavuvi na familia zao
Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa
wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, Jumatatu tarehe 19 Novemba 2012 amefungua
Kongamano la ishirini na tatu la utume wa bahari, linalowajumuisha wajumbe mia nne
kutoka katika nchi sabini wanaounda Familia ya Utume wa Bahari.
Hili ni kongamano
kubwa kuwahi kuandaliwa na Baraza la kipapa. Itakumbukwa kwamba, makongamano mengine
yamefanyika nchini Poland kunako mwaka 2007, Brazil 2002, Ufilippini 1997, Marekani
1992. Wajumbe wanarudi tena mjini Vatican baada ya kupita takribani miaka thelathini
walipokutanika hapa kwa mara ya kwanza, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka
tisini tangu hati juu ya Utume wa Bahari ilipopitishwa na Papa Pio wa kumi na moja.
Ni utume ambao ni muhimu sana kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.
Makleri,
watawa na waamini walei wamekabidhiwa dhamana ya kuinjilisha kwa njia ya utume wa
bahari, changamoto inayokwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Imani na agizo lililotolewa
na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya, iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini
Vatican.
Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, kila mwanadamu anapata fursa
ya kusikiliza Habari Njema ya wokovu ikitangazwa kwake, licha ya umbali na vikwazo
vinavyoweza kujitokeza. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya sekta ya safari za majini
na uvuvi yameleta athari na changamoto katika maisha na kazi kwa mabaharia na wavuvi,
lakini zaidi wakati huu wa myumbo wa uchumi kimataifa. Licha ya magumu na changamoto
hizi, lakini ubaharia ni fursa nyingine inayoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika Uinjilishaji,
anasema Kardinali Vegliò.
Vyombo vya usafiri majini vinabeba si tu mizigo na
bidhaa, bali watu kutoka katika kila lugha, jamaa na taifa, watu ambao wanalazimika
kuwa mbali na Familia na Jumuiya zao za Kikristo bila hata ya kupata lishe ya imani
yao. Uinjilishaji Mpya sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawawezeshe wahudumu
wa utume wa bahari kuboresha imani yao, kwa kuamini Habari Njema ya Wokovu, tayari
kutoka kifua mbele ili kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao
ya Kikristo unaojidhihirisha katika uwepo, huduma na mshikamano endelevu.
Huduma
ya upendo haina budi kuwakumbatia mabaharia wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, kwani
ushuhuda wa upendo kwa mabaharia wanaoteseka na kunyanyasika ni kielelezo makini cha
mshikamano wa Kristo kwa wote. Kanisa linawapongeza kwa mchango na majitoleo yao.
Kongamano hili ni fursa ya kusikiliza, kushirikishana na hatimaye, kutekeleza dhamana
hii nyeti kwa moyo wa upendo na mshikamano.
Kardinali Antonio Maria Vegliò
anawashukuru wafadhili na viongozi mbali mbali ambao wameendelea kuwa ni mfano bora
wa kuigwa katika utoaji wa huduma kwa mabaharia. Amehitimisha hotuba yake ya ufunguzi
kwa sala iliyotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili katika Waraka wake wa kichungaji,
Kanisa Oceania.