2012-11-19 08:20:17

Uharibifu wa tabaka la Ozone una madhara makubwa kwa binadamu


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao makuu yake mjini Geneva, hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa ishirini na nne wa nchi wanachama, uliokuwa unajadili mambo yanayochangia kuharibika kwa Tabaka la Ozone, kama sehemu ya utekelezaji wa itifaki ya Montreal, inayoadhimisha kumbu kumbu ya miaka ishirini na mitano tangu ilipotiwa sahihi na nchi wanachama.

Askofu mkuu Tomasi anabainisha kwamba, kipindi cha miaka ishirini na mitano ni muda muafaka kabisa wa kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu maendeleo yaliyokwishafikiwa tangu Itifaki ya Montreal ilipotiwa sahihi, ili kulinda Tabaka la Ozone lenye umuhimu sana katika maisha ya mwanadamu na utunzaji wa mazingira. Uharibifu wa Tabaka la Ozone unaweza kuwa na madhara makubwa katika maisha ya mwanadamu, jambo linalohitaji uwajibikaji wa pamoja, wa ajili ya mafao na maendeleo ya kizazi hiki na kile kijacho.

Kuna haja kwa nchi wanachama wa Itifaki ya Montreal kushirikiana na wadau wengine katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira, kwa kushikamana pamoja ili kuzisaidia nchi zinazoendelea duniani ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ili kwa pamoja ziweze kuchukua hatua madhubuti katika kutunza mazingira.

Dhamana ya kulinda na kutunza mazingira inakwenda sanjari na haki msingi za binadamu, kwani madhara yake ni makubwa kwa afya za wananchi walio wengi. Kwa nchi changa duniani, itakuwa ni vigumu kwao kuweza kupata tiba ya magonjwa yanayosababishwa na uharibifu wa Tabaka la Ozone kutokana na gharama za matibabu haya kuwa ni kubwa. Ikumbukwe kwamba, kuongezeka kwa kina cha maji baharini kumepelekea mamillioni ya watu kuyakimbia makazi yao pamoja na kudumaza uchumi wa maeneo husika.

Utunzaji wa Tabaka la Ozone kiwe ni kielelezo cha mshikamano kwa kizazi hiki na kile kijacho. Katika kipindi cha miaka ishirini na mitano iliyopita, kumekuwepo na mafanikio ya kuridhisha katika kutunza na kuhifadhi Tabaka la Ozone, kutokana na Serikali kushirikishana maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kupashana habari pamoja na kukazia elimu ya utunzaji bora wa mazingira., lengo ni kuwajibika kikamilifu katika utunzaji wa kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuifanya kwa hekima na busara.

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu unabainisha kwamba, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kuhimiza utunzaji bora wa mazingira kwa kukazia elimu ya mazingira, kanuni za maadili, matumizi bora ya vitu kwa kuepuka ulaji wa kupindukia kwa kutambua kwamba, mazingira ni zawadi kubwa kwa maisha na ustawi wa mwanadamu, yanapaswa kulindwa na kutunzwa vyema.

Binadamu ajenge utamaduni wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya mafao yake; juhudi hizi zijioneshe kwa kuwa na sera na sheria makini zinazoheshimiwa na kutekelezwa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anahitimisha mchango wake kwa kusema kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni wajibu fungamanishi kwa familia nzima ya binadamu, unapania kukuza na kudumisha maendeleo yake, kwa sasa na kwa wakati ujao.








All the contents on this site are copyrighted ©.