2012-11-19 08:23:03

Onesheni ukomavu na uzalendo kwa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu


Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana katika mkutano wao wa mwaka uliohitimishwa hivi karibuni linawaalika wananchi wa Ghana kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu nchini humo utakaofanyika tarehe 7 na tarehe 28 Desemba 2012, ili kumchagua rais pamoja na wabunge, watakaopewa dhamana ya kuiongoza nchi ya Ghana.

Maaskofu wanawaomba wagombea urais na ubunge pamoja na mashabiki wao, kuhakikisha kwamba, wanadumisha misingi ya haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa. Upande utakaoshindwa uoneshe ukomavu na uzalendo wa kukubali matokeo kwa heshima na taadhima, kwani katika mashindano yoyote kuna kushinda na kushindwa.

Wagombea nafasi za uongozi wawaelimishe wananchi madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa kama uchaguzi hautazingatia: sheria, kanuni na maadili mema. Wapiga kura wajiepushe na vitendo vya kudanganya pamoja na kuwapigia kura hata wale waliokwisha kufariki, kwani vitendo vya namna hii vinaweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa. Wale watakaoshinda waupokee ushindi wao kama heshima na dhamana kutoka kwa wananchi wa Ghana na wale watakaoshindwa waoneshe uzalendo kwa kukubali matokeo kwa heshima na taadhima wanasema Maaskofu, ikiwa kama uchaguzi utakuwa ni huru na wa haki.

Wabunge watakaochaguliwa kutoka katika vyama vya upinzani, hata katika uchache wao, lakini watambue kwamba, wanayo dhamana kubwa kuchangia mawazo chanya katika uendeshaji wa shughuli za Serikali. Wabunge wote kwa pamoja watambue kwamba, lengo la kuu ni kwa ajili ya kutafuta mafao ya wa wananchi wa Ghana katika ujumla wao na hivyo wawe tayari kupokea tamko rasmi kutoka katika Tume ya Uchaguzi Ghana.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, linavitaka vyombo vya habari na vyama vya siasa kutoa nafasi kwa Tume ya Uchaguzi Ghana kutekeleza wajibu na dhamana yake kwa kutangaza kwa wakati muafaka wale watakaoibuka washindi baada ya uchaguzi, vinginevyo wanaweza kusababisha vurugu na ghasia zisizo na msingi wala tija kwa wananchi wa Ghana. Pale ambapo sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi hazikufuatwa kikamilifu, vyama vya siasa na mashabiki wao, watumie sheria za nchi kutafuta haki yao msingi bila kukimbilia vurugu na fujo.

Maaskofu wa Ghana wanasema, mara baada ya washindi kutangazwa, wananchi wanapaswa kuachana na tofauti zilizowagawa wakati wa mchakato wa kupiga kura, ili kushikamana kwa pamoja kujenga na kuimarisha misingi ya mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ghana. Wananchi wajenge umoja na mshikamano wa kitaifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.