Kanisa ni sauti ya Kinabii inayotangaza Kweli za Kiinjili ili kukabiliana na changamoto
mbali mbali zinazojitokeza ndani ya Jamii
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 17 Novemba 2012 alikutana na kuzungumza
na Kundi la Pili kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, lililohitimisha hija
yao ya kitume inayofanyika kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican.
Baba
Mtakatifu anasema, Kanisa ni mjumbe wa Neno la Kristo lenye mguso na utambulisho wa
kidini, lakini linafumbata ndani yake hekima ya Kimungu inayoweza kusaidia kupata
ufumbuzi wa matatizo na changamoto mbali mbali zinazoikumba Jamii katika ulimwengu
wa utandawazi. Wakristo wanaalikwa kuwashirikisha jirani zao sauti ya matumaini, inayosubiriwa
kwa hamu kubwa.
Baba Mtakatifu anasema, Ufaransa ina historia yenye utajiri
mkubwa ambayo kamwe haiwezi kubezwa wala kutwezwa. Kanisa lina dhamana na wajibu wa
kuhakikisha kwamba, sauti yake inasikika, hata kama Kanisa na Serikali inatekeleza
wajibu na dhamana yake katika ngazi mbili tofauti zinazopaswa kuheshimiwa, lakini
ikumbukwe kwamba, Kanisa lina dhamana ya kutangaza Ukweli unaokomboa na kujaza mioyo
ya watu matumaini na mapendo ya dhati.
Baba Mtakatifu anawaalika Waamini walei
wanaotekeleza utume wao katika maisha ya hadhara kuendelea kushirikiana na Maaskofu
kusimama kidete dhidi ya sheria zinazoweza kuhataraisha misingi ya maisha ya ndoa
na familia inayoundwa kati ya Bwana na Bibi. Ni wajibu wao kutangaza Injili ya Uhai
tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti inapomfika kadiri
ya mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu anaungana na Maaskofu Katoliki Ufaransa
kuonesha wasi wasi wake unaojikita katika urithishaji wa imani kwa vijana wa kizazi
kipya; changamoto zinazoendelea kuzikabili familia nyingi ambazo kimsingi zinahitaji
kupatiwa msaada ili kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo.
Kuna baadhi
ya watu wanataka kudhalilisha dhamana na utume wa Kanisa, ili uonekane kuwa ni jambo
binafsi; changamoto kwa waamini kutolea ushuhuda wa imani yao kifua mbele, daima wakisukumwa
na ujasiri, uaminifu na mafundisho adili ya Kanisa. Hii ndiyo changamoto endelevu
katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Wazazi watekeleze wajibu wa malezi kwa watoto
wao na kwa ajili ya mafao ya wengi.