2012-11-19 08:16:41

Kanisa linapania kuwajengea wahudumu wa sekta ya afya utamaduni wa kupenda zawadi ya maisha!


Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahudumu wa sekta ya afya anabainisha kwamba, mkutano wa ishirini na saba wa afya kimataifa, uliokuwa umeandaliwa na Baraza la Kipapa, uliohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican, ulipania kuwajengea wafanyakazi wa sekta ya afya utamaduni wa kulinda na kutunza afya ya wagonjwa kwa njia ya majiundo makini: kimaadili, kiroho na kiutu.

Ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanasoma alama za nyakati, ili kutoa tiba muafaka kwa wagonjwa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na utu wake. Kwa wafanyakazi wa sekta ya afya ndani ya Kanisa Katoliki wanapaswa kutambua kwamba, huduma yao haina budi kupata chimbuko lake katika imani na maadili, kanuni na sheria na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kusimama kidete kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kukua na kukuzwa siku hadi siku.

Ilikufikia lengo hili, kuna haja ya wafanyakazi wa sekta ya afya ndani ya Kanisa kuwa na majiundo makini si tu katika taaluma yao, bali wanapaswa pia kupata mafunzo ya maadili ya Kikristo katika kuwahudumia wagonjwa, ili waweze kutekeleza dhamana hii, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao wenye mvuto na mguso, unaoweza kuwa ni chemchemi ya Uinjilishaji Mpya.

Hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ziwe ni mahali pa Uinjilishaji Mpya, kwa kusimama ridete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kuongozwa na maadili na utu wema, dhidi ya utamaduni wa kifo, ambao umemgeuza mwanadamu kuwa si mali kitu! Ni matumaini ya wajumbe walioshiriki katika mutano huu kwamba, watatekeleza changamoto hii wanaporudi katika vituo vyao vya kazi, tayari kushiriki katika huduma ya upendo wa Kristo unaokomboa.








All the contents on this site are copyrighted ©.