2012-11-19 08:03:40

Hati ya huduma ya kichungaji kwa watumiaji wa barabara Barani Afrika baada ya Kongamano la Kimataifa lililofanyika Dar Es Salaam, Tanzania


Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kuanzia tarehe 11 hadi 15 Septemba 2012, liliendesha Kongamano la Kimataifa kwa kuongozwa na kauli mbiu iliyochukuliwa kutoka katika sehemu ile ya Injili ya Luka inayowaonesha Wanafunzi wa Emmaus walipokuwa wanatembea njiani kutoka Yerusalemu “Yesu mwenyewe alikaribia akaandamana nao” kwa kuwahusisha wajumbe themanini na mbili kutoka katika nchi thelathini na moja Barani Afrika. RealAudioMP3

Wajumbe wa mkutano walipata fursa ya kusikia ujumbe wa matumaini kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, aliyewatia shime na ari ya kusonga mbele kwa matumaini ili kubaianisha mikakati itakayoweza kutumiwa na Kanisa katika shughuli zake za kichungaji miongoni mwa watumiaji wa barabara.

Mkutano huu ulihudhuriwa pia na Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na Madhehebu ya Kikristo walioshiriki kama wageni waalikwa. Tamko la mkutano huu, linabainisha kwamba, wajumbe walifurahia upendo na ukarimu uliooneshwa na watanzania wakati wote walipokuwa wanashiriki katika mkutano wao.

Itakumbukwa kwamba, Kongamano hili ni mwendelezo wa Makongamano ya Kimataifa yaliyowahi kufanyika huko Amerika ya Kusini, kunako mwaka 2008; Barani Ulaya mwaka 2009na Asia pamoja na Oceania kwama 2010. Mkutano huu ni matunda na changamoto kutoka katika Waraka wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, Dhamana ya Afrika, Africae Munus, anayewachangamotisha waamini Barani Afrika kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa.

Kwa namna ya pekee, Kongamano hili lilijikita zaidi katika masuala yanayowagusa: wanawake, vijana na watoto. Wawakilishi kutoka nchi mbali mbali Barani Afrika walionesha utekelezaji wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watuamiaji wa barabara. Walipembua kwa umakini mkubwa hali ya usalama wa barabara Barani Afrika, utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Walikazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa elimu kwa madreva ili waweze kubadili tabia kwa kukazia heshima, nidhamu, uaminifu na busara wanapotekeleza majukumu yao. Wajumbe walizungumzia pia utu na heshima ya wanawake, wasichana na watoto bila kusahau dhamana ya familia katika Jamii.

Wajumbe hawa kwa pamoja walimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapatia fursa ambayo imewawezesha kufungua akili na mioyo yao ili kuona shida na mahangaiko ya watumiaji wa barabara Barani Afrika, ili kuibua mwongozo utakaosaidia utekelezaji wa shughuli na mikakati ya kichungaji.

Wanatambua kwamba, Bara la Afrika ni mahali ambapo kuna mamillioni ya watu wanaosafiri kwa hiyari yao wenyewe au kwa kulazimishwa kutokana na sababu mbali mbali, kiasi kwamba, barabara na mitaa hii inakuwa ni fursa inayoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kila mtu anapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa; kupata haki na mahitaji yake msingi, kama ambavyo walibainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Dhana ya uhamaji ina madhara makubwa katika masuala ya kifamilia, kijamii na kiuchumi, ingawa wajumbe wanatambua kwamba, Familia ya Kiafrika ni mahali pa kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kimaadili, daima wakiongozwa na mafao ya wengi.

Wajumbe wamesikitisha na baadhi ya: mila na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati, zinazoendelea kusababisha nyanyaso na madhulumu kwa wanawake na watoto. Vijana wengi wanakabiliwa na baa la njaa, magonjwa, dhuluma, ukosefu wa heshima na utu wao na hata wakati mwingine, kifo; mambo yanayosababishwa na baadhi ya wananchi, serikali na kudumaa kwa uchumi na maendeleo Barani Afrika.

Licha ya ukweli kwamba, biashara haramu ya utumwa imefutwa Barani Afrika, lakini hadi leo hii kuna utumwa mamboleo, dhuluma, nyanyaso, ubaguzi, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na biashara ya ngono ambayo inaendelea kukua na kupanuka sehemu mbali mbali duniani, kiasi cha kuwatumbukiza watu katika utumwa mamboleo.

Mwingiliano wa watu ni jambo jema, lakini umekuwa pia ni sababu ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ukimwi, unaotokana na watu kufanya kazi kwa muda mrefu, ukosefu wa mapumziko, ukosefu wa miongozo ya maisha ya kiroho, rushwa na vitendo vya jinai. Umaskini, dhuluma na nyanyaso, kinzani na migogoro ya kifamilia, mila potofu ni kati ya mambo yanayopelekea wasichana wengi kujitumbukiza katika biashara ya ngono na watoto kujikuta wanaishi katika mazingira hatarishi.

Wajumbe wanapongeza juhudi mbali mbali zilizofanywa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na huduma kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi. Wanasema, kuna haja ya kuongeza juhudi za majadiliao ya kidini na kiekumene katika kuwahudumia watumiaji wa barabara katika ngazi mbali mbali Barani Afrika. Wanatambua kwamba, dhamana ya Kanisa kwanza kabisa ni Kuinjilisha, kuelimisha na kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili.

Wajumbe kwa dhati kabisa wanapendekeza kwamba, Kanisa liendeleze huduma ya kichungaji kwa watumiaji wa barabara, kwa kukazia usalama barabarani na ukombozi wa wanawake na wasichana kutoka katika biashara na utumwa wa ngono pamoja na kuwalinda watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kushirikiana katika ngazi mbali mbali: Kimataifa, Kikanda, Kijimbo na Kiparokia.

Kanisa Barani Afrika lianzishe miundo mbinu itakayoliwezesha kutoa elimu makini ili kupambana na nyanyaso kama hizi. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa utamadunisho Barani Afrika, kukazia utawala wa sheria na utekelezaji wake; kuwaandaa wahudumu watakaojitoa kimaso maso kuwahudumia watumiaji wa barabara Barani Afrika. Shule na taasisi za elimu ziinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa ziwe ni mahali pa kuzuia nyanyaso na madhulumu kama haya. Viwepo vituo vya utoaji wa ushauri nasaha.

Kanisa Barani Afrika lijikite zaidi katika Uinjilishaji Mpya kwa kuangalia maeneo mapya yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Watawa washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama njia ya kutambua na kuthamini mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kudumisha pia ushirikiano miongoni mwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika. Waandaliwe viongozi wa kiroho watakaowahudumia kiroho watumiaji wa barabara.

Mshikamano wa dhati unaoongozwa na kanunu ya auni uliwezeshe Kanisa Barani Afrika kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi. Vijana waandaliwe vyema ili kukabiliana vyema na maisha yao, daima wakiwa wanawajibika katika maisha yao wenyewe na kwa jirani zao.








All the contents on this site are copyrighted ©.