2012-11-19 08:27:22

Gusweni na mateso pamoja na mahangaiko ya wagonjwa mnaowahudumia!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe 18 Novemba 2012 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa ajili ya wajumbe wa Kongamano la ishirini na tano la kitaifa kwa ajili ya Shirikisho la Madaktari Wakatoliki kutoka Italia. Kongamano hili lilianza hapo tarehe 15 na kuhitimishwa hapo tarehe 18 Novemba, 2012 hapa mjini Roma.

Katika mahubiri yake, Kardinali Bertone amewakumbusha wajumbe hao kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini na tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, inaonekana kuwa na maneno makali yanayoweza kuleta hofu na wasi wasi miongoni mwa waamini, lakini Injili ya Kristo inapania kuleta mabadiliko ya ndani, kama sehemu ya mchakato wa ukamilifu wa mpango wa Mungu katika historia, kwa kuyaweka yote chini ya Kristo.

Ni mwaliko wa kujiandaa vyema kwa ajili ya ujio wa pili wa Kristo, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, akiwa na nguvu na utukufu, tofauti kabisa na ilivyojitokeza katika Fumbo la Umwilisho, anapojionesha katika hali ya umaskini. Yesu atakuja kuwakusanya watu wake, ili waweze kushiriki katika utukufu walioandaliwa na Baba yake tangu milele yote na kwamba ufalme wake hautakuwa na mwisho. Huu ni mwanga wa matumaini na maisha ya kweli.

Kardinali Bertone anawakumbusha Madaktari kwamba, wanahitaji Neno la uzima ili waweze kutekeleza kwa ukamilifu zaidi wito na utume wao, unaowapatia fursa ya kukutana na watu wanaoteseka, ili waweze kwanza kabisa, kuwaonjesha upendo, kuguswa na mahangaiko ya wagonjwa wanaowahudumia kwa moyo na akili yote. Upendo kwa wagonjwa uwawezeshe kuwapatia faraja kwa njia ya uchunguzi na tiba kamili, daima wakiongozwa na fadhila ya imani, mapendo na matumaini. Wafanyakazi katika sekta ya afya wasukumwe zaidi na utu wema wanapotekeleza wajibu wao kwa wagonjwa badala ya kuangalia tu taaluma yao kama wanavyobainisha Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Madaktari watambue kwamba, wanashiriki utume wa Kanisa unaowawajibisha kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kushiriki katika kazi ya ukombozi, wakiongoza na heri za mlimani, muhtsari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake. Kutokana na dhamana hii, sehemu yao ya kazi inakuwa ni jukwaa la kujitakatifuza na kuwatakatifuza wengine, daima wakijitahidi kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba. Imani na dhamiri nyofu, viwawezeshe wahudumu katika sekta ya afya kutekeleza dhamana yao kwa unyofu na uchaji mkuu.

Ni matumaini ya Kardinali Tarcisio Bertone kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yatawasaidia wafanyakazi katika sekta ya afya kuyaumia kama kipindi cha neema, kinachowangamotisha kuwa wabunifu zaidi wanapotekeleza wajibu wao, wakiongozwa na kweli za Kiinjili, ili wawe ni mashahidi na wainjilishaji.

Kongamano la madaktari hawa limewawezesha kupembua changamoto za kimaadili zinazoendelea kuibuka katika tiba mintarafu imani yao ya Kikristo Barani Ulaya. Udaktari ni taaluma ambayo kwa sasa inakabiliana na changamoto ya utamaduni wa kifo unaojionesha katika sera, tamaduni, elimu, haki na katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, yote haya yanawasukuma kwenda kinyume kabisa cha Injili ya Uhai.

Wafanyakazi wa sekta ya afya watambue na kuthamini utume wao wa kinabii, kwa kutolea ushuhuda thabiti ili kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha na kutetea ukweli bila ya kuangalia makunyanzi. Wafanyakazi Wakristo katika sekta ya afya wanapaswa kuwa upande wa Injili ya maisha, wakitumia taaluma yao kwa ajili ya kulinda na kuokoa maisha ya watu na wala si kinyume chake.

Dhamana hii inawahitaji madaktari ambao wanapenda kusimama kidete kulinda na kutetea uhai kwa kuendelea kuwa waaminifu katika taaluma yao, kwani wao ni watangazaji wa Injili ya uhai na matumaini; ni Wasamaria wema wanaojitaabisha kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa katika mahangaiko yao, kwa kudumisha haki na upendo, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.








All the contents on this site are copyrighted ©.