"Sitisheni mashambulizi ya Makombora kwa ajili ya mafao ya pande hizi mbili"
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, ameonesha masikitiko
yake makubwa kutokana na mgogoro wa kivita unaoendelea kufuka moshi kwenye Ukanda
wa Ghaza na Israel. Anazitaka pande zote mbili kuacha uhasama na kuhakikisha kwamba,
wanatoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.
Mgogoro wa kivita katika maeneo
haya unaendelea kusababisha vifo na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia. Kuna idadi
kubwa ya watu ambao wamejeruhiwa vibaya sana, wengi wao ni wanawake na watoto. Baraza
la Makanisa Ulimwenguni linafuatilia kwa umakini mkubwa mwenendo mzima wa mgogoro
huo ambao umeibuka kwa kasi kubwa na kutaka pande zote mbili kusitisha mara moja mapigano
ili kuokoa maisha ya watu.
Binadamu ana thamani kubwa machoni pa Mwenyezi
Mungu na kwamba, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, hayawezi kukubalika kama malipo
kutokana na migogoro na kinzani na migogoro ya kisiasa na kivita ambayo bado haijapata
ufumbuzi wake.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaliomba Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa pamoja na Shirikisho la Nchi za Kiarabu kutafuta suluhu ya haraka
ili kuhakikisha kwamba, vita hii inasitishwa kwa ajili ya mafao ya pande zote mbili.
Dr. Tveit anasema kuwa, ni jambo ambalo halikubaliki kuona wananchi wanaoishi
Israel wakishambuliwa na makombora kutoka Ukanda wa Ghaza, kwani mwelekeo huu unaweza
kuhatarisha harakati za Palestina kutaka kutambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama
Nchi huru.