2012-11-17 15:21:38

Sayansi ya Kikristo juu ya mateso inafumbatwa katika: mguso, mshikamano, majitoleo ya dhati na kushirikishana


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe17 Novemba 2012, aliwapongeza wajumbe wa mkutano mkuu wa ishirini na saba wa afya kimataifa uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Hospitali, mahali pa Uinjilishaji: utu wa kiutu na kiroho; sanjari na wajumbe wa kongamano la Shirikisho la Madaktari Wakatoliki Italia na Ulaya, waliokuwa wanajadili kuhusu maadili ya kibayolojia na "Ulaya ya Kikristo", bila kusahau umati mkubwa wa wagonjwa na wanafunzi wataalam katika sekta ya afya waliokuwa wanahudhuria pia mikutano hii kama sehemu ya majiundo yao.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linawaangalia wagonjwa na wote wanaoteseka kwa moyo na upendo wa kidugu; likisukumwa na roho ya Kristo ambaye kwa njia ya Fumbo la Mateso yake ameyapatia mahangaiko ya mwanadamu utu na mwelekeo mpya, kwa kutambua kwamba, ni watu ambao si pweke na utu wao una thamani kubwa, kwani, wanaunganisha mateso na mahangaiko yao katika Msalaba wa Kristo, kama sehemu ya ushiriki wao katika mateso yanayookoa.

Kutokana na mwaliko huu, Kanisa linapenda kuwawashia wataalam wa sekta ya afya na watu wanaojitolea moyo wa matumaini, kwa kutambua kwamba, wana wito maalum kabisa, unaowawajibisha kujifunza kwa bidii, juhudi na maarifa; kwa kuguswa na kutafuta mang'amuzi mapana zaidi. Wote wanaojitosa kimasomaso katika wito huu, watambue kwamba wanashiriki utume wa maisha ya kiutu na kiroho unaozidi hata vyeti vya taaluma walivyopokea.

Hii ni Sayansi ya Kikristo juu ya Mateso, inayobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kama ukweli pekee unaotoa jibu makini katika Fumbo la Mateso pamoja na kujitahidi kuwahudumia kwa ufanisi mkubwa. Si wajibu wa Kanisa kuwapatia afya bora wala kuwapunguzia mateso yao, lakini wanayo zawadi kubwa ambayo ni Kristo aliyeshiriki Fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu, kielelezo cha ajabu kabisa cha thamani ya mateso ya mwanadamu.

Wafanyakazi katika sekta ya afya ni wataalam waliobobea katika Sayansi ya Mateso ya Mwanadamu. Utambulisho wao wa Kikatoliki unawapatia wajibu na dhamana nyeti sana ndani ya Jamii na Kanisa; huu ni wito wa pekee kabisa kama ambavyo wamedhihirisha watakatifu kama vile: Giuseppe Moscati, Mtakatifu Ricardo Pampuri, Mtakatifu Gianna Beretta Mola, Mtakatifu Anna Schaffer pamoja na Mtumishi wa Mungu Jèrome Lejeune.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, wakati huu wa Uinjilishaji Mpya na myumbo wa uchumi kimataifa, kuna haja ya kutafuta rasilimali zitakazoweza kusaidia kulinda na kutetea afya; hospitali, vituo vya afya vinapaswa kuwa ni mahali pa kudumisha mafao ya wengi na kamwe afya isifanywe kuwa ni bidhaa kwa ajili ya wateule wachache ndani ya Jamii.

Utu n a heshima ya wagonjwa vilindwe na kudumishwa na kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba yasaidie kutoa tiba ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuzingatia kanuni, maadili na utu wema, kwani wito wa Madaktari ni kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu katika kila hatua ya maisha yake hapa duniani.

Sayansi ya Kikristo kuhusu mateso inajikita zaidi kwa mtu kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zake; mshikamano, majitoleo, kushirikishana, ili hatimaye, kuwa ni walimu wa kweli kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Maneno ya Msamaria mwema yawe ni msingi thabiti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa maadili na utu wema.

Kutokana na mwelekeo kama huu, Hospitali inakuwa ni mahali pa Uinjilishaji, kwani ni mahali hapa ambapo Kanisa linaonesha kwa namna ya pekee kabisa uwepo wa Mungu kwa kuthamini na kujali utu na heshima ya binadamu. Kiini cha huduma zinazotolewa na sekta ya afya ni binadamu katika hali zake zote, binadamu anayehitaji kulindwa na kushirikishwa maana ya Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu.

Mgonjwa aonje uhusiano wa utume wa upendo anapokuwa Hospitalini, mahali ambapo upendo wa Msamaria mwema unajionesha kwa namna ya pekee kabisa kwa kutambua pia kuwa sura ya mgonjwa ni sura ya Kristo. Wafanyakazi katika sekta ya afya wanakabiliwa na utume wa kutoa tiba na kuinjilisha kwa kutambua kwamba, ulimwengu mamboleo unahitaji sana Wasamaria wema, watu wenye moyo wa ukarimu na wanaonyoosha mikono yao tayari kuwakumbatia wote, kwa kutambua kwamba, huu ni wajibu ambao ni kipimo cha huduma yao kwa Jamii.

Ni huduma kama hii inayopita uwezo wa mwanadamu, inayotekelezwa na Makleri na Watawa katika sekta ya afya, ili kuhakikisha kwamba, Fumbo la Mateso ya mwanadamu linapata mwanga kutoka kwa Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaambia wagonjwa kwamba, ukimya wao ni ushuhuda makini katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya, wale wanaowatibu na kuwahudumia kwa matumaini kwamba, hakuna hata chozi la mtu awaye yote litakalopotea bure machoni pa Mwenyezi Mungu.

Wagonjwa ni ndugu zake Kristo katika mateso yao na kwamba, kwa njia ya mateso yao wanashiriki katika wokovu wa dunia. Baba Mtakatifu anawaweka wagonjwa na wafanyakazi wote katika sekta afya chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria afya ya wagonjwa, ili aweze kuongoza mapito yao, daima wakiwa ni mashahidi wa Sayansi ya Kikristo kuhusu mateso.







All the contents on this site are copyrighted ©.