2012-11-16 08:31:31

Rais Thomas Boni Yayi na Kardinali Polycarp Pengo kushiriki katika semina ya kimataifa iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani, Roma


Kanisa Barani Afrika "Ecclesia in Africa" na Dhamana ya Afrika "Africae Munus" ni hati mbili zilizotolewa na Mama Kanisa baada ya maadhimisho ya Sinodi mbili zilizojikita katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, zimekuwa ni changamoto kwa wasomi ndani na nje ya Bara la Afrika kuendelea kufanya tafiti za kina, ili kushirikisha zaidi na zaidi mchango wa Kanisa Barani Afrika katika kumwendeleza mwandamu kiroho na kimwili.

Kwa mara ya pili, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani, kilichoko hapa mjini Roma, kimeandaa semina ya kimataifa, itakayowashirikisha viongozi wa Kanisa na Kisiasa kutoka Barani Afrika, watakaozungumzia kuhusu tafiti kutoka Afrika kuhusu mapambano dhidi ya baa la umaskini, majiundo makini, ujasiriamali, utawala na uongozi bora. Semina hii ya kimataifa itafanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani, Jumatatu, tarehe 19 Novemba 2012.

Rais Thomas Boni Yayi wa Benin ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na atazungumzia kuhusu "Sera ya Maendeleo Barani Afrika mintarafu mipango ya Umoja wa Afrika". Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagscar ambaye pia ni Rais wa heshima kimataifa katika tafiti za maendeleo ya utamaduni wa Mwafrika atatoa neno wakati wa semina hii.

Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum na Askofu mkuu mteule Fortunatus Nwachuku ni kati ya viongozi wandamizi kutoka Vatican wanaotarajiwa kushiriki katika semina hii ambayo inaingia awamu ya pili.

Hizi ni juhudi za Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani kutaka kuwahamasisha wasomi na wanazuoni ndani na nje ya Bara la Afrika, kujikita katika tafiti, zitakazosaidia mchakato wa kuthaminisha utamaduni kutoka Bara la Afrika kama njia kuliendeleza Bara la Afrika, ili watu wake wasigenishwe na tamaduni kutoka nje zinazoingia kwa kasi kwa njia ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wasomi wanahamasishwa kufanya tafiti za kina, ili kulipatia Bara la Afrika: utu na heshima yake katika Jumuiya ya Kimataifa mintarafu mchango wa Kanisa Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.