Rais Alassane Ouattara akutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu mjini Vatican
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Ijumaa tarehe 16 Novemba amekutana na kuzungumza
na Rais Alassane Ouattara wa Pwani ya Pembe mjini Vatican. Viongozi hawa wawili wamezungumzia
uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Pwani ya Pembe, sanjari na mchango wa Kanisa
Katoliki katika mchakato wa maendeleo endelevu nchini humo.
Wamesema, Kanisa
bado linaweza kuchangia zaidi katika kuimarisha na kusimamia misingi ya haki, amani,
majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na upatanisho wa kitaifa, chachu muhimu
sana katika jitihada za wananchi kujiletea maendeleo yao.
Baba Mtakatifu pamoja
na Rais Outtara wanasema, kuna haja kwa Kanisa na Serikali kuendelea kushirikiana
kwa karibu zaidi hususan katika utoaji wa huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo
endelevu. Viongozi hawa kwa pamoja wameonesha nia ya kutiliana sahihi mkataba wa ushirikiano
baina ya nchi hizi mbili.
Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamegusia
pia changamoto zinazojitokeza Barani Afrika, kwa kuzingatia kwamba, kwa sasa Rais
Ouattara ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi Afrika Magharibi, ECOWAS.
Rais
Ouattara na ujumbe wake, walikutana na ujumbe wa Vatican uliokuwa unaongozwa na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.