2012-11-16 07:57:41

Mama Kanisa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Crescencia kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 17 Novemba 2012


Mtumishi wa Mungu Maria Crescencia Pèrez aliyeishi kati ya Mwaka 1897 hadi mwaka 1932 ni kutoka katika Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Orto. Kutangazwa kwake kuwa Mwenyeheri ni furaha isiyokuwa na kifani kwa Kanisa zima, lakini kwa namna ya pekee, kwa Familia ya Mungu nchini Arjentina, inayoshuhudia Binti yao akiandikwa kwenye Kitabu cha Watakatifu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akatika Barua yake ya kichungaji kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Crescenzia Pèrez kuwa Mwenyeheri anasema kwamba, ni mtawa ambaye amejitahidi katika hija ya maisha yake hapa duniani kumwilisha Injili ya Upendo katika hali ya kawaida, kwa unyenyekevu na upendo usiokuwa na makuu.

Ni mtawa aliyekuwa na utulivu wa ndani na furaha ya kweli katika hija ya maisha yake, ndiyo maana watu wengi hadi leo hii wanamwita “Sista Mpendelevu” “Sor Dulzura”. Mashahidi wengi wanasema, kwa hakika watawa wote walikuwa ni wema, lakini Sista Maria Crescencia Pèrez alikuwa ni mwema zaidi kuliko wengine wote. Ni mtawa aliyekuwa na utashi thabiti, mvumilivu, mwema, mwenye furaha na mpendelevu.

Tabia hii iliboreshwa zaidi kwa njia ya Imani hai, isiyotetereka; Imani ambayo ilimwilishwa katika matendo na uhalisia wa maisha ya kila siku. Shughuli zake za kichungaji na kitume zilipata chimbuko lake katika Imani, kiasi kwamba, alionekana kana kana kwamba, ni mtu ambaye aliishi hapa duniani, lakini moyo wake ulikuwa mbinguni, kama anavyosimulia moja wa mashahidi wake.

Upendo wake, anasema Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa lenye dhamana ya kuwatangaza Watakatifu na Wenyeheri, aliyekabidhiwa dhamana ya kumwakilisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Ibada ya kumtangaza kuwa Mwenyeheri kwamba, ni mtawa ambaye upendo wake, ulijionesha kwa namna ya pekee, kwa Mungu na jirani.

Alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, si tu kwa maneno matupu, bali kwa jasho na bidii ya kazi ya mikono yake, kwa kuwalipia wale waliokuwa hawana mavazi, watoto wagonjwa ambao wazazi wao walishindwa kulipia gharama za dawa.

Alitoa maziwa kwa wagonjwa, akiwaonesha upendo mkamilifu. Kwa watoto waliokuwa wanapokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza, alihakikisha kwamba, kila mtoto anafurahia kwa kuwa na nguo nzuri, kwa kuwapatia vitabu vya kumbu kumbu na rozari, ili kila mtoto aweze kweli kuifurahia siku hii ambayo alikuwa anakutana na Yesu wa Ekaristi katika maisha yake.

Daima alisikika akisema kwamba, Yesu Kristo anajidhihirisha kwa namna ya pekee miongoni mwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, hawa wanapaswa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Kardinali Angelo Amato anasema, kutangazwa kwa Mtumishi wa Mungu Maria Crescencia Pèrez kuwa Mwenyeheri, ni mwaliko kwa waamini kukuza na kuimarisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maisha yao pamoja na kuwashirikisha wengine bila woga wala makunyanzi. Ni changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa sala, huduma kwa wagonjwa na maskini; kwa watoto na wenye kuhitaji.

Ni mtawa anayehimiza tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu; upendo wa kidugu na furaha inayobubujika kutoka katika Imani. Mtawa huyu ni kielelezo bora cha utu wema, utulivu na amani ya ndani; furaha na upendo mkamilifu. Ni cheche ya upendo wa Mungu inayoburudisha moyo wa mwanadamu na kumsukuma kutafuta lililojema zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.