2012-11-16 07:26:51

Lengo na makusudi ya mchakato wa utamadunisho ni kumpatia mwamini uzima wa milele!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika mfululizo wa makala juu ya Utamadunisho, Padre Nikodemo Mayala anaendelea kupembua dhana hii kwa ufasaha mkubwa. Leo kwa namna ya pekee, anapembua utamadunisho kama lengo la kupata uzima wa milele. RealAudioMP3

Ladha ya utamadunisho. Sasa ladha ya utamadunisho imefufuka. Watu wanamrudia Mungu. Kazi tuliyonayo nyumbani ni utafiti jinsi tumwelewavyo Mungu sisi, kwa fikira, lugha, na mwono wetu. Na si jinsi myahudi ajuavyo ulimwengu, myunani ajuavyo ulimwengu au mzungu au mwasia ajuavyo ulimwengu na Mungu. Lengo ni kupata uzima wa milele, “na uzima wa milele ndiyo huu: wakujue Wewe, Mungu wa pekee na wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma”(Yn.17:3).

Afrika tunatambua kuwa Mungu ni kiini cha maisha yetu. Twanuia kutengeneza Familia ya Mungu. Ni wazi ukoloni ulituwekea mipaka na uadui, na kuuwa udugu. Lakini mipaka hii bandia haikuvunja tunu zetu za asili. Hivi utamadunisho waufikisha ufufuko wa Kristo nyumbani. Hata katika siasa nyumbani hatukufungamana na mtu peyote.

Tulikiri na kuamini: Binadamu wote ni ndugu zangu, na Afrika ni moja. Katika maongezi , lugha ya wingi huwezi kuiepa. Magharibi hii haipo. Utasikia mimi, na si sisi. Mimi nasema, na si sisi tunasema. Tunahitaji mapinduzi ya fikira maana kwa bahati mbaya ubinafsi huu sasa, nyumbani umefika. Fisadi yu jikoni.

Changamoto katika kutamadunisha. Utamadunisho ni swala gumu linalohitaji uangalifu, umakini, busara na uhodari mkubwa. Awali linaibuliwa swali kuhusu uaminifu wa Kanisa kwa Injili na urithi na mapokeo ya kitume katika kukua kwa tamaduni mbalimbali. Hatuna budi kuzingatia upatanifu, utangamanifu, hali ya kuchukuana na ujumbe wa injili tukikumbuka kuwa lila la fila havitangamani. Pili , kuenzi mwungano na mshikamano na kanisa la ulimwengu. Ndiyo, kutunza umoja, ushirika na kanisa la kristo.

Hivi, utamadunisho wajuzu maisha ya Kanisa na hatua za uinjilishaji. Hii yahusu, taalimungu, (teolojia), taaliyote, (falsafa), liturujia, maisha ya kanisa na miundo yake yote. Kumbe, utafiti wa kina lazima ufanyike. Changamoto kuu ni mapinduzi toka utamaduni wa mgeni kwenda utamaduni wa mkazi. Upeo wa mgogoro, kilele cha mgogoro ni kuua umimi. Wasiwasi mkuu upo katika dhana hii ya kung’ang’ania changu na ndoto ya kale, hamu ya nyumbani, hamu ya mambo tuliyozoea, ya kale dhahabu, enzi zetu.

Sasa tusiongozwe tu na mazoea bali ufahamu , maarifa mapya, fasiri sahihi na aminifu kwa Mungu na watu. Tuzingatie tena wosia wa Mtume Paulo: “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmevaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani.

Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”(Gal.3:26-28). Hitaji kubwa ni mapinduzi ya fikira, kujenga uaminifu na uwezo. Mzizi uliong’olewa ni vigumu kuurejesha katika uhalisia wake.








All the contents on this site are copyrighted ©.