2012-11-16 08:58:59

Kanisa Katoliki nchini Kenya bado limesimama kidete kulinda na kuwatetea wanyonge na wote wanaokandamizwa!


Askofu Anthony Muheria wa Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya anasema, Kanisa Katoliki nchini Kenya bado limesisima kidete kulinda na kutetea maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake ambao kimsingi ni sauti ya kinabii, ambayo wakati mwingine haipokelewi kwa mikono miwili.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya vyombo vya habari vinaiangalia "kwa jicho la makengeza" sauti ya Kinabii inayotolewa na Kanisa kwani kwao habari za Kanisa si mali kitu!

Ni jukumu la vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya maadili, utu wema, na uwajibikaji unaopania maendeleo ya wengi na kamwe wasitekwe na wanasiasa kwa ajili ya mafao yao binafsi wala kutegemea "kikandamiza habari" ili habari za Kanisa ziweze kuandikwa ili zisomwe, zisikilizwe au kutazamwa na watu wengi zaidi. Kanisa nchini Kenya, linawachangamotisha waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kushirikiana na Kanisa kwa karibu zaidi kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao.

Kanisa kwa upande wake, linaahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linapania kutekeleza wajibu wake wa kinabii katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya mwaka 2013.

Kanisa linatoa mwongozo makini unaopaswa kufuatwa na wengi ili kupata viongozi waadilifu, wachapakazi, waaminifu na wachamungu, watakaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kenya katika ujumla wao.

Kanisa halitawafumbia macho wanasiasa wanaotaka kuwagawa wananchi kwa misingi ya ukabila na udini kwani mwelekeo kama huu ni hatari na unaweza kusababisha maafa makubwa, kama ilivyowahi kujitokeza nchini Kenya wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Wananchi wajitokeze kujiandikisha kwa wingi na kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi, kama sehemu ya utekelezaji wa haki yao kikatiba.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linaendelea kuutafakari muswada wa sheria kuhusu ndoa, ili kuiangalia katika mapana yake, likizingatia kwa namna ya pekee, dhamana na maisha ya ndoa; haki msingi za binadamu pamoja na haki za wanawake wanaokubali kuolewa katika ndoa ya wanawake wengi nchini humo, bila kusahau haki za watoto. Maisha ya ndoa na familia si jambo la mchezo: lina wajibu na dhamana kubwa kwa mtu binafsi na katika Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.