Viongozi waandamizi simamieni kikamilifu miradi ya maendeleo ili kuleta tija
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya waachane na dhana ya
“Eyes on Hands Off” kama kweli wanataka kusukuma mbele maendeleo ya nchi hii kwani
dhana hiyo imechangia mambo mengi kukwama.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Alhamisi,
Novemba 14, 2012) wakati akifungua Mkutano Maalum wa Kazi wa siku tatu kwa Wakuu wa
Mikoa na Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ulioanza leo kwenye ukumbi wa Pius Msekwa
mjini Dodoma.
“Ninatoa rai kwenu kujaribu kuondokana na tafsiri isiyokuwa sahihi
ya dhana ya “Eyes on Hands Off” kuwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya hatakiwi kuingilia
utendaji wa walio chini yake hata kama hawatekelezi vema wajibu wao na hivyo kusababisha
mambo kutokwenda”, alisema.
“Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wewe ndiwe Rais
amekuteua na kukukabidhi madaraka ya kusimamia eneo lako. Kauli hii isiwaondolee jukumu
la kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu. Ni lazima mkaitembelee
na kujua kinachoendelea,” alisema huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu alisisitiza
kwamba: “Hii ni dhana potofu lazima sasa tuachane nayo. Lazima tufanye kazi kwa karibu
na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo katika maeneo tunayoyasimamia inatekelezwa
kwa ukamilifu.”
Aliwakumbusha viongozi hao kwamba Serikali imeandaa Mpango
wa Taifa wa Maendeleo muda mrefu na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 -2016)
ambao imeanza kuutekeleza.
“Viongozi mliopo hapa ni chachu muhimu sana ya kusimamia
utekelezaji wa mipango hiyo. Tunahitajika kuandaa kwa kina na kusimamia utekelezaji
wa mipango yetu kwa kuanisha wajibu wa kila mmoja katika utekelezaji... tunatakiwa
kupanga na kusimamia matumizi ya fedha zinazotolewa kwa kuzingatia vipaumbele vichache
tunavyokubaliana. Hatua hii itaonesha haraka matokeo mazuri na makubwa kwa maeneo
ya kipaumbele na hatimaye kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao kwamba Serikali kwa sasa ina mkakati
mzuri wa kutambua mchango wa wabunifu na wagunduzi katika kuendeleza sayansi na teknolojia.
“Tumepitisha sheria ya kuwatambua wagunduzi hivi karibuni, hivyo, tuna sehemu ya kuanzia,”
aliongeza.
Aliwataka Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya pamoja na Makatibu Tawala
wa Mikoa wafanye kazi ya kuwabaini na kuwaendeleza wagunduzi wanaopatikana katika
ngazi za Mikoa na Wilaya, ili kazi zao zisaidie kuendeleza uchumi wa Tanzania.
Akifafanua,
Waziri Mkuu alisema Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa ujulikanao kama
“Global 2013 Smart Partnership Dialogue” ambao utafanyika jijini Dar es Salaam Mei
24 – 28, 2013 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akihudhuria
mkutano kama huo huko Petrojaya, Malaysia, Juni 2011.
“Kwa kutambua kazi kubwa
iliyoko mbele ya maandalizi ya mkutano huo mkubwa, jukumu lenu kubwa ni kusimamia
mchakato mzima wa maandalizi ya Mkutano wa kitaifa kuanzia ngazi ya Wilaya na Mikoa,”
alisisitiza.
Alisema wao ni Wenyeviti wa Mabaraza ya Biashara katika ngazi
za mikoa na wilaya. Hivyo, baada ya mkutano huo wanatakiwa kuitisha mikutano ya mabaraza
na kuendesha kwa kina midahalo muhimu katika ngazi zenu ili matokeo ya midahalo hiyo
itumike kwenye mdahalo wa kitaifa ifikapo Januari 2013.
“Tujitahidi kati ya
sasa na Januari 2013 tuwe tumekusanya maoni ya kutuwezesha kushiriki kwenye Mkutano
huo. Jukwaa hili la Kimataifa liwe sehemu ya kupanua ushirikiano wa kimataifa katika
nyanja ya teknolojia na ubunifu. Wanachotaka kwetu sisi kabla ya kwenda kwenye mkutano
huo lazima tuwe na makundi tayari ya kuchangia” alisisitiza.
Mikutano ya “International
Smart Partnership Dialogue” huandaliwa na nchi mwenyeji ikishirikiana na Taasisi ya
Jumuiya ya Madola iitwayo Commonwealth Partnership for Technology Management – CPTM
yenye makao yake jijini London, Uingereza. Mikutano hii ambayo hufanyika kila baada
ya miaka miwili, ilianza kufanyika mwaka 1995, na ilipewa msukumo mkubwa na Waziri
Mkuu Mstaafu wa Malaysia, Dkt. Mahathir Mohammed.
Mikutano hii huendeshwa
kwa ushirikiano kati ya Malaysia na Nchi za Kusini mwa Afrika zikiwemo Zimbabwe, Zambia,
Botswana, Msumbiji, Swaziland na Lesotho. Uganda imekuwa mwenyeji wa mikutano hii
mara mbili mwaka 2001 na 2009.
Mikutano ya “Smart Partnership Dialogue” tofauti
na mikutano mingine ni jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na jumuiya mbalimbali
za wananchi kuhusu jambo lo lote lenye manufaa kwao na ambalo litachangia kuleta maendeleo
yao kijamii na kiuchumi. Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo wa ngazi za juu
hukaa pamoja kama watu wa ngazi sawa na jumuiya za wananchi, zikiwemo za vijana, wasomi,
wafanyakazi, wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanasanaa na utamaduni, wanasiasa
na madhehebu ya dini.
Naye Prof. Lucien Msambichaka wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) akitoa mada kuhusu ushirikiano kwa manufaa ya wote (Smart Partnership Dialogue)
alisema hapa nchini kuna wabunifu na wagunduzi wenye vipaji mbalimbali ambao wanapaswa
kuendelezwa ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aliwataja baadhi
yao kuwa wapo waliobuni ndege (Arusha), trekta (Ruvuma), incubator (Dar es Salaam),
antenna za tubelight (Temeke-DSM), madish ya televisheni (Mbeya), na na kusisitiza
kuwa wote hawa wanahitaji kuwezeshwa kiteknolojia ili kuboresha viwango vya vifaa
walivyovibuni. “Wakipatiwa nguvu ya teknolojia, itawasaidia katika kuwezesha ukuaji
shirikishi wa kijamii na kiuchumi,” alisema Prof. Msambichaka.
Akizungumzia
kuhusu ukuaji wa kiuchumi, aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao wanashiriki mkutano
huu wasimamie maendeleo katika maeneo yao ili Tanzania iweze kweli kufikia malengo
yake ya kuwa ni Taifa lenye uchumi wa kati (middle income country) ifikapo mwaka 2025.
Mada
nyingine zitakazowasilishwa kwenye mkutano huo wa siku tatu ni Hali ya Usalama wa
Nchi; Usimamizi na Ufuatiliaji wa shughuli za Serikali hususan Miradi ya Maendeleo;
Usimamizi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Serikali za Mitaa na Usimamizi na Ufuatiliaji
wa shughuli za Serikali za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mada nyingine ni
Migogoro ya Ardhi; Maandalizi ya Msimu wa Kilimo 2012/2013; Hali ya Lishe Nchini pamoja
na Umuhimu Bima ya Afya kwa Wananchi.