Kuna mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika majadiliano ya kiekumene tangu
baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo, anasema
kuwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, ilikuwa ni fursa
ya pekee kuweza kukutana na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, wote kwa pamoja wakipania kwanza kabisa: kusali, kutafakari
pamoja na kushirikishana uzoefu, mang’amuzi, matatizo, changamoto mbali mbali zinazojitokeza
katika maeneo yao, ili kuandaa mwongozo utakaoliwezesha Kanisa kujikita katika Uinjilishaji
kama njia ya kutangaza Imani yake.
Ni matatizo na changamoto ambazo kila nchi
inapoyaangalia inadhani kwamba ni yake, lakini kuna uhusiano mkubwa na kile kinachoendelea
sehemu mbali mbali za dunia.
Anabainisha kwamba, katika kipindi cha miaka
hamsini tangu maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na maendeleo
makubwa katika majadiliano ya kiekumene, hususan katika lile Tamko la pamoja kuhusu
“Mafundisho juu ya kuhesabiwa haki, lililotolewa Mwezi Agosti 1999, kati ya Kanisa
la Kiluteri na Kanisa Katoliki. Kuna haja ya kuendelea kukazia majadiliano ya kiekumene
hasa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ili kuwa ni uelewa na mtazamo unaolielewa
Kanisa na Wakatoliki katika mapana yake. Kwa pamoja wanapaswa kutambua jambo ambalo
ni kiini cha Kanisa.
Majadiliano ya kiekumene yanaendelea kujionesha hata miongoni
mwa waamini wa Kanisa Anglikani, ambao kutokana na msukumo wao pamoja na busara ya
kichungaji iliyooneshwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, baadhi yao wamekubaliwa kujiunga na Kanisa Katoliki, huku wakiendeleza Ibadan
a tamaduni za Kanisa Anglikani.
Majadiliano ya kiekumene yanaendelea pia miongoni
mwa waamini wa Kanisa la Kiothodox, lakini bado kuna haja ya kuelewa dhana ya Uongozi
wa Sinodi na Mfumo wa Uongozi ndani ya Kanisa hili.
Kardinali Kurt Kocha anabainisha
kwamba, kuibuka na kukomaa kwa tabia na dhana ya ukanimungu ni matunda yaliyojitokeza
kwa namna ya pekee katika kipindi cha Karne ya kumi na sita, ambako Makanisa yalipigana
na kushambuliana kwa misingi ya Imani, kiasi cha kuwakatisha tamaa wale waliokuwa
wanapenda kujiunga na Ukristo, kwani kama Ukristo ulikuwa unajitambulisha kwa njia
ya “mtutu wa bunduki” basi kulikuwa hakuna haja ya kujiunga na Kanisa, ambalo kimsingi
lilipaswa kuwa ni mtetezi na msimamizi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
wa kweli.
Kumbe, hali ambayo mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia amefikia ni matunda ya mabadiliko ya kihistoria na vipaumbele
vya maisha ya mwanadamu, kiasi cha kumfanya kutoona umuhimu wa uwepo wa Mungu katika
maisha yake, hitimisho ambalo ni hatari kabisa, kwani bila uwepo wa Mungu, mwanadamu
si mali kitu, utu na heshima yake viko hatarini. Hii ndiyo changamoto kubwa katika
dhamana ya Uinjilishaji Mpya.
Kardinali Kurt Kocha anasema kwamba, Maadhimisho
ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uwe ni mwendelezo wa mabadiliko
ya dhati yaliyopaniwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hakuna mpasuko
katika utekelezaji wa mabadiliko ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, kunako mwaka
2005 alibainisha mwendelezo wa Mabadiliko yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa
Vatican.