Kumbu kumbu ya miaka 10 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo II alipotembelea Bunge la Italia
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano, tarehe 14 Novemba 2012 amewatumia
ujumbe wa matashi mema viongozi na wabunge wa Seneti ya Italia wakati wa maadhimisho
ya miaka kumi tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipotembelea bungeni hapo tarehe
14 Novemba 2002. Hili lilikuwa ni tukio muhimu sana katika harakati za kuimarisha
uhusiano kati ya Vatican na Serikali ya Italia, licha afya ya Baba Mtakatifu Yohane
Paulo wa pili, wakati ule kuwa imeanza kudhohofu. Wabunge walimpokea kwa heshima na
taadhima na kwamba, hotuba aliyoitoa inaacha chapa ya kudumu katika mioyo na akili
za watu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na kardinali Tarcisio
Bertone, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa na Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu
msaidizi wa Vatican.
Miaka kumi imepita, lakini katika hotuba yake, Mwenyeheri
Yohane Paulo wa pili alikuwa amewachangamotisha Wabunge nchini Italia, kuhakikisha
kwamba, wanajichotea utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Mapokeo ya Kikristo, ambayo
kwa namna ya pekee, yanawapatia utambulisho wao: kijamii na kitamaduni pamoja na kuendeleza
dhamana yake katika Umoja wa Ulaya na Ulimwengu kwa ujumla.
Aliwataka kwa
namna ya pekee kabisa, kutumia urithi wao wa maisha ya kiroho na kimaadili katika
kutafuta mafao ya wengi na hasa zaidi wanapokabiliana na changamoto katika utekelezaji
wa majukumu yao, ili kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na wananchi.
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, kuna haja ya kuendeleza ushirikiano kati
ya Vatican na Italia; kati ya Kanisa na Serikali, ili Italia iweze kutekeleza wajibu
na dhamana yake kwa kuenzi familia mahali pa elimu na makuzi ya kijamii; kila mwananchi
akijitahidi kutekeleza wajibu wake ndani ya Jamii. Baba Mtakatifu anawahakikishia
uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka kwa ajili ya ufanisi na tija katika huduma kwa
wananchi wa Italia.
Askofu mkuu Angelo Becciu anasema kuna uhusiano mkubwa
kati ya siasa na maadili, kwani demokrasia isiyozingatia tunu msingi za maisha ya
kimaadili na utu wema ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya nchi; adui mkubwa katika
maisha ya kiroho na kisiasa nyakati hizi ni utovu wa nidhamu, ukosefu wa maadili pamoja
na watu kupenda kujikita katika mawazo mepesi mepesi.
Kwa upande wake, Kardinali
Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anabainisha kwamba, maadili
na utu wema hayana budi kuwa ni dira na mwongozo katika utungaji wa sheria ambazo
kimsingi zinapaswa kuzingatia haki. Ili kufikia lengo hili, wanasiasa wanapaswa kweli
kuwa na dhamiri nyofu inayoongozwa na sheria maadili. Ni wajibu wa wanasiasa kulinda
na kuzitegemeza familia, hasa katika harakati za kuwapatia watoto wao elimu bora.