2012-11-15 12:15:55

Hospitali ni mahali pa Uinjilishaji kwa njia ya huduma ya mapendo kwa wagonjwa


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 15 Novemba 2012 amefungua mkutano wa ishirini na saba wa afya kimataifa, ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, unaoongozwa na kauli mbiu: Hospitali mahali pa Uinjilishaji: utume wa kiutu na kiroho.

Amewapatia wajumbe hao salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Kardinali Bertone, katika mahubiri yake amekazia kwamba, mbegu ya Ufalme wa Mungu imekwisha kupandwa kati yao na inaendelea kukua, ili iweze kuzaa matunda kwa wakati wake: ni mwaliko kwa waamini kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, dhamana ambayo wanataaluma katika sekta ya afya wanaishiriki pia. Ufalme wa Mungu unapokelewa katika ukweli, unyenyekevu na uwajibikaji wenye tija, pamoja na kuvunja vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kukwamisha uhuru wa Watoto wa Mungu unaowawajibisha kwa jirani zao.

Mkutano huu wa ishirini na saba wa afya kimataifa, unafanyika mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, mwaliko kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, Hospitali pia zinatumika kama sehemu maalum ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na utoaji wa huduma makini kwa wagonjwa. Uzoefu, mang'amuzi, changamoto na matatizo watakaoshirikishana wakati wa mkutano wao ni mambo ambayo yanaweza kuwa ni msaada mkubwa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linaalikwa kwa namna ya pekee, kufuata nyayo za Kristo, kwa njia ya huduma kwa binadamu, kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili. Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati ni mahali ambapo wagonjwa wanakimbilia ili kupata tiba ya magonjwa na faraja katika maisha yao ya kiroho; kumbe ni mahali muafaka kabisa kwa ajili ya kutangaza Ufalme wa Mungu.

Kardinali Bertone anawakumbusha wafanyakazi katika sekta ya afya kwamba, shida na mahangaiko ya mwanadamu ni mahali pa kukuza na kuimarisha matumaini, kwani mwanadamu ameumbwa mwili na roho. Tumaini la Kikristo ni hatua kubwa katika tiba ya mwili na mwelekeo katika maisha ya uzima wa milele. Kanisa linatambua kwamba, ni nyenzo ya huduma makini kwa binadamu, kama ambavyo alikwisha wahi kusema Mama Teresa wa Calcutta.

Ni vyema ikiwa kama maboresho ya tiba yanakwenda sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini daima mtu anapaswa kuwa ni kiini cha tafiti na maendeleo haya na wala si kinyume chake. Maadili, utu na heshima ya binadamu vinapaswa kuzingatiwa katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa; waguswe zaidi na mateso na mahangaiko ya wagonjwa, daima wawe tayari kuwaonjesha upendo wa dhati wagonjwa.

Kama kuna jambo la kujivunia anasema Kardinali Bertone, basi, wahudumu wa sekta ya afya wajivunie kutoa huduma ya upendo na faraja kwa wagonjwa. Ikumbukwe kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kuhusu kweli za kiimani na huduma ya upendo wa wagonjwa, changamoto kwa wahudumu wa sekta ya afya kutumia vipaji na karama zao kwa ajili ya maboresho ya huduma kwa wagonjwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.