2012-11-14 09:50:23

Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakutana Kigali, Rwanda ili kufanya hija ya matumaini, ili kuleta mabadiliko katika sura ya nchi!


Vijana wa Jumuiya ya Taize iliyoanzishwa na Fra Roger kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, kuanzia tarehe 14 hadi 18 Novemba 2012 wanashiriki katika mkutano ambao ni kielelezo cha hija ya matumaini duniani.

Mkutano huu pia unawashirikisha baadhi ya wajumbe kutoka Ulaya, Amerika na Asia, lengo la vijana hawa ni kumwadhimisha Kristo, wakifanya hija ya pamoja kwenye chechemi ya matumaini inayopania kuleta mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na Jamii kwa ujumla.

Ni muda muafaka kwa vijana kutoka Eneo la Maziwa Makuu kuweza kuishi kwa pamoja, katika hali ya amani, upendo na mshikamano wa kweli; wakishirikishana mang'amuzi na vipaumbele vya maisha ya Kikristo, katika uwanja wa kitaifa na kimataifa; daima wakijitahidi kuonesha dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa, katika mchakato wa kujenga na kuimaarisha matumaini na amani miongoni mwa waamini wa dini zao.

Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakutanika nchini Rwanda, ambako Mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari, zaidi ya watu laki nane walipoteza maisha yao kutokana na chuki za kikabila. Tangu wakati huo, juhudi za pamoja zinaendelea kufanyika kwa kujikita katika mchakato wa msamaha na upatanisho wa kweli, kila mwananchi akijitahidi kutumia vipaji na karama alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuijenga nchi yake akipania kutafuta mafao ya wengi, kulinda na kusimama kidete kutetea haki msingi za binadamu.

Vijana wanasema wako nchini Rwanda si kwa ajili ya kuwasuta Wanyarwanda, wala kujadiliana yale yaliyopita, bali kujenga utamaduni wa kusikiliza na kuimarisha utashi wa vijana katika harakati za kuboresha maisha yao kiroho na kimwili, wakiheshimiana na kuthaminiana kama watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Vijana wanafanya tafakari ya kina kuhusu vyanzo vya imani yao, Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo, muhtasari wa imani ambayo inawaunganisha vijana hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Vijana wanasema, kwa pamoja wanapenda kuonja upendo mkamilifu wa Kristo, ambao una nguvu zaidi kuliko kifo na ubaya wa binadamu.

Vijana wanapenda kukutana na kuzungumza na wale ambao wameshuhudia utamaduni wa kifo ukigusa undani wa maisha ya Wananchi wa Rwanda; kuwasikiliza wale ambao kimsingi wamesimama imara kulinda na kutetea haki, amani na mshikamano wa kitaifa; kushirikiana kwa karibu zaidi na wote wanaoendeleza kuhimiza ukweli, upatanisho na msamaha, unaopata chimbuko lake katika toba na wongofu wa ndani.

Kwa hakika wanasema viongozi wa Jumuiya ya Taizè, vijana wanataka kusoma Injili ya Upendo na Mshikamano, ulioneshwa kwa namna ya pekee kwa njia ya Msalaba wa Kristo pale mlimani Kalvari.







All the contents on this site are copyrighted ©.