2012-11-14 12:15:09

Mshikamano wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kwa wananchi wa Syria


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum hivi karibuni, amehitimisha ziara ya kichungaji nchini Lebanon, alikokuwa ametumwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kama kielelezo cha mshikamano wake na wananchi wa Syria wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na kupamba moto kwa mtutu wa bunduki, kiasi kwamba, watu wengi wanalazimika kuyakimbia makazi yao na wengine wanaendelea kupoteza maisha yao.

Kardinali Sarah alipata nafasi ya kuweza kukutana na kuzungumza na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza utume wake nchini Lebanon, Syria, Jordani, Uturuki na Iraq. Kwa pamoja wameangalia miradi ambayo itagharimiwa na msaada wa dolla za kimarekani millioni moja zilizotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa ajili ya watu wanaoteseka nchini Syria kutokana na vita pamoja na kinzani za kisiasa na kijamii.

Kardinali Sarah anasema, wananchi wa Syria katika ujumla wao wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko yao, kiasi cha kuonesha moyo wa huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Msaada uliotolewa utasaidia juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika harakati za kuwahudumia wakimbizi kutoka Syria wanaoishi katika mazingira magumu na hali ya kutisha, lakini wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto.

Watu wengi wamekata tamaa kutokana na mgogoro huu kuendelea kufuka moshi kwa kasi kubwa zaidi bila ya wananchi kufahamu hatima yake ni nini! Wakimbizi wanahitaji anasema Kardinali Sarah: huduma ya maji safi na salama, nishati, chakula na mavazi, kwani kuna watu walilazimika kuyakimbia makazi yao bila kuchukua kitu chochote wakihofia usalama wa maisha yao. Mchango uliotolewa na Baba Mtakatifu ni kidogo sana ikilinganishwa na matatizo wanayokabiliana nayo.

Lengo ni kuonesha mshikamano wa Kanisa na watu hawa katika mahangaiko yao ya ndani. Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ili kuwsaidia wakimbizi na wahanga wa vita na migogoro huko Mashariki ya Kati, kwa tumaini kwamba, iko siku: haki, amani na utulivu vitaweza kushika mkondo wake.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutekeleza wajibu wake, kwa kuhakikisha kwamba, vita, kinzani na migogoro inakoma huko Mashariki ya Kati na kwa namna ya pekee, huko Syria ambako hali inaendelea kuwa mbaya zaidi. Ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.