2012-11-14 09:11:54

Lengo la Uinjilishaji Mpya katika Ulimwengu mamboleo


Mpendwa msiklizaji wa Radio Vatican, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu kabisa katika mfululizo wa vipindi vyetu vya uinjilishaji wa kina ambapo tunaendelea kuiangalia kwa pamoja Mwongozo wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni. Juma hili tupige hatua mbele kidogo kuangalia juu ya kukutana na kuungana na Kristo ambalo ndilo lengo msingi la uinjilishaji. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakumbusha kwa mara nyingine tena juu ya utume msingi wa Kanisa lilipokea toka kwa Kristu mwenyewe yaani kuhubiri injili kwa mataifa yote na kuwafanya wote kuwa wanafunzi wa Yesu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI analikumbusha Kanisa kuwa Utume lililokabidhiwa na Yesu mwenyewe kimsingi ni utume unaolidai na kulituma Kanisa kuihubiri na kuifundisha Injili kama Yesu mwenyewe alivyoihubiri akingali katika ulimwengu huu.

Tena analifananisha Kanisa na Mtume Paulo ambaye alisema wazi kuwa yeye ni Mtume aliyewekwa wakfu na Yesu Mwenyewe kwa ajili ya kutangaza ujumbe wa Kristo. Hivyo anamalizia Baba Mtakatifu kuwa kazi ya Kanisa si kufundisha Biblia au vifungu vyake bali kuutangaza ujumbe wa Kristo katika namna kwamba watu wa Mungu waweze kuuishi ujumbe huo.

Injili, Baba Mtakatifu Benedikto XVI anafafanua kuwa ni Kristu mwenyewe anayeongea na watu wake ndani ya Kanisa. Kumbe Kanisa lina utume wa kumtangaza Kristu anayejidhirisha siku hadi siku katika neno lake daima akiwaonesha watu wake njia sahihi ya kuenenda, akiwaokoa kwa lile tumaini analolitoa katika neno lake juu ya ufalme wa Mungu na kuwapatia uzima wa milele pale watu wake watakapomsikia na kumwendea yeye.

Kwa msaada na maongozi ya Roho Mtakatifu wampokeaye wale wanaomsikia Kristu na kumwamini wanapata uzima na kuokoka na yule mwovu na kuwa mashahidi wa Kristu kwa wengine.

Kuhubiri Injili kumbe ni kujenga mazingira, mahali na mwanga kwa wanafamilia ya Mungu kumjua Kristu, kumpokea katika maisha yao kama Bwana na Mwokozi wao, kumpenda na kumtumikia yeye siku zote. Kwa maneno mengine ni kujenga mazingira mazuri ya watu wa Mungu kukutana uso kwa uso na Yesu katika neno lake na sakramenti zake na kuungana naye kabisa katika Imani. Waamini kwa uinjilishaji mpya wanapaswa kuwezeshwa kukutana na Yesu katika neno lake na kuungana naye katika Ekaristi Takatifu.

Makutano haya baina ya muumini na Yesu mwenyewe ni nafasi pekee ambapo waumini wanapata kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kuonja muungano wa Yesu na Mungu Baba. Yesu anamdhihirisha Baba kwa viumbe wake na tena anawaleta wafuasi wake kwa Baba. Katika mapana yake Uinjilishaji mpya ni ujenzi wa mazingira kwa utangazi wa imani ambayo si inafikiriwa tu bali waamini wanaishuhudia kwa maisha yao ya kila siku, wanaiadhimisha katika ibada, wanaisali na kuuiishi katika mazingira halisi ya ulimwengu huu wa leo.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anakazia na kulitaka Kanisa kujifunga kibwebwe katika suala zima la uinjilishaji mpya na hivyo anawataka Maaskofu katika Sinodi kujipanga vizuri kwa zoezi hili. Anasema kutanga imani ni jambo kubwa linaloleteza wajibu mkubwa kwa upande wa watangazaji wa imani. Kanisa halina budi kuwa mfano wa maisha ya imani, maisha ya ushuhuda wa ujumbe wa Kristo.

Baba Mtakatifu anasema sio rahisi kutangaza imani kwa wengine wakati mtangazaji mwenyewe haamini na haishi kulingana na imani anayoitangaza. Hivyo changamoto kwa Kanisa kujizatiti kiimani na kimapendo yaani kumvaa Kristu mwenyewe ili likisimama na kupunga bendera ya Kristu basi lionekane kweli mpiga debe wa Kristo.

Anaendelea kubainisha kuwa utume huu wa kutangaza imani ueleweke vizuri miongoni mwa wanakanisa hivi kwamba kila mbatizwa ahusike moja moja katika uinjilishaji mpya. Maana yake hizi si zama za kusimama mimbarini bali kumtangaza Kristo kwa maisha ya ushuhuda: kwa matendo yetu ya imani na upendo tumdhihirishe Kristo kwa mataifa yote.

Kanisa linaalikwa kupitia waumini wake kuushuhudia upendo upeo wa Kristo usio na mipaka kwa mataifa. Kile alichofanya Yesu mwenyewe ndicho wanakanisa wanapaswa kukiendeleza katika ulimwengu wa leo; kufukuza pepo wachafu, kuponya magonjwa na kuwajali wahitaji wa kila hali.

Mpendwa msikilizaji hadi hapa tumefika mwisho wa kipindi chetu kwa siku ya leo. Nakutakia kila Baraka na kheri kutoka kwa Mungu Baba, nikikuaga kutoka studio za Radio Vatican ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.









All the contents on this site are copyrighted ©.