Kwa ushuhuda wa Imani katika matendo, waongozeni wengine kumfahamu na kumpenda Mwenyezi
Mungu aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano tarehe 14 Novemba 2012, katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ameendelea kutafakari kwa kina kuhusu hamu ya kukutana
na Mwenyezi Mungu ambayo inajikita katika undani wa moyo wa mwanadamu. Kwa njia ya
neema yake, Mwenyezi Mungu anaandamana na mwanadamu katika harakari za kumfahamu ili
hatimaye, aweze kujipatia furaha ya kweli katika maisha yake.
Baba Mtakatifu
anasema, leo hii katika ulimwengu mamboleo, inasikitisha kuona kwamba, Imani inaonekana
kuwa ni jambo gumu sana, kiasi cha mwanadamu kufikiri na kudhani kwamba, anaweza kuishi
bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anapoondolewa
katika maisha ya mwanadamu, anakumbana na utupu, kwani utu na heshima ya mwanadamu
ni matokeo ya kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwaliko wa kujishikamanisha na Mungu.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini popote pale walipo kuhakikisha kwamba, wanatoa sababu
makini juu ya Imani na Matumaini yao. Sababu hizi zinajikita kwa namna ya pekee katika
kazi ya uumbaji inayoonesha utukufu wa Mungu Muumbaji; hamu ya maisha ya uzima wa
milele ambayo imejificha katika undani wa moyo wa mwanadamu, hamu ambayo inapata kitulizo
chake mbele ya Mwenyezi Mungu peke yake; na katika imani ambayo inaangaza na kuleta
mabadiliko katika maisha ya mwanadamu, kwa kuungana na Kristo kila siku ya maisha
yao.
Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya ushuhuda wa Imani katika matendo,
waamini wanaweza kuwaongoza wengine kumfahamu na kumpenda Mwenyezi Mungu aliyejifunua
kwa njia ya Yesu Kristo Mkombozi wa dunia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, ametambua uwepo wa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa ishirini na saba
kimataifa amboa umeandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili
ya wafanyakazi katika sekta ya afya. Amewashukuru pia wanakwaya wa Kwaya ya Kanisa
kuu la Westeminster kutoka Uingereza bila kuwasahau mahujaji kutoka sehemu mbali mbali
za dunia.
Ametambua uwepo wa washiriki wa kongamano lililoandaliwa na Shirikisho
la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja
na washiriki wa kozi maalum iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani.
Anawakumbusha kwamba, hija yao kwenye Makao Makuu ya Mtakatifu Petro, yaamshe ndani
mwao ari na mwamko wa toba ili kushiriki kwa dhati dhamana ya Uinjilishaji Mpya.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewatakia kila neema na baraka wakati Mama
Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Alberti Mkuu, Msimamizi wa wachongaji na
wanasayansi asilia, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Novemba