Mwanadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya ulinzi na usalama
Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za
Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni ameshiriki katika mkutano wa
kimataifa uliokuwa unajadili kuhusu silaha zenye uwezo wa kuleta maafa na madhara
makubwa kwa binadamu.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu, umeonesha hofu
kubwa kutokana na madhara yanayoweza kusababishwa na silaha hizi kwa kuzingatia usalama
wa kitaifa. Kuna milipuko mikubwa ya silaha ambayo haidhibitiwi wala kutolewa taarifa
na wakati mwingine, silaha hizi zinaangukia mikononi mwa magaidi na hatari yake inakuwa
ni kubwa zaidi, kiasi hata cha kugusa kinzani na migogoro ya kisiasa inayoendelea
kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia. Umakini wa itifaki ya tano na utekelezaji
wake, iko mashakani, ingawa hili lingepaswa kuwa ni lengo la Jumuiya ya Kimataifa.
Askofu
mkuu Tomasi anaendelea kusema kwamba, kuna haja kwa Serikali husika kuweka takwimu
sahihi za matumizi ya silaha zenye madhara makubwa pamoja na kushirikisha taarifa
zake mara baada ya kinzani na migogoro kumalizika, kwani kushindwa kutekeleza wajibu
huu, madhara yake ni makubwa kwa binadamu. Kutakuwa na mauaji ya watu wasiokuwa na
hatia, madhara makubwa katika uchumi na maisha ya Jamii husika pamoja na kudumaza
maendeleo ya watu.
Utekelezaji wa awamu ya tatu hauna budi kuanza mara moja
anasema Askofu mkuu Tomasi, ili kufahamu fika kiasi cha silaha kilichopo pamoja na
kuanza harakati za kusafisha maeneo ambayo kimsingi yameathirika kutokana na uwepo
wa silaha hizi za mahangamizi, kwani utekelezaji huu, ni sehemu ya uwajibikaji kimaadili.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendeleza ushirikiano huu, ili kumwilisha
utifaki katika mataifa mengi zaidi duniani, ingawa kimsingi utekelezaji wake ni mgumu,
lakini hakuna haja ya kukata tamaa. Ujumbe wa Vatican unaungana na Chama cha Msalaba
Mwekundu, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine kuonesha masikitiko yake
makuu kutokana na nchi nyingi kushindwa kuridhia itifaki hii, ambayo inalenga kulinda
na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwa kuzingatia sheria ya kimataifa.
Mwanadamu
anapaswa kuwa ni kipaumbele cha kwanza katika masuala ya ulinzi na usalama na kwamba,
raia wapewe ulinzi wa kutosha. Inasikitisha kuona kwamba, katika kinzani na vita inayoendelea
kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia, wanaopoteza maisha yao kwa wingi ni raia wasiokuwa
na hatia, hali inayoonesha kwamba, kimsingi hakuna utii wa sheria za kimataifa.
Ni
wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatoa ulinzi wa kutosha kwa raia
na mali zao dhidi ya milipuko ya silaha wakati na mara baada ya vita. Raia wana haki
ya kuishi katika mazingira salama, yenye amani na utulivu bila kuwa na wasi wasi wa
vitisho vya milipuko ya silaha za mahangamizi.