2012-11-13 10:59:54

Mfuko wa Mo Ibrahim wamtunukia Tuzo Maalum Askofu mkuu Desmond Tutu kwa kusimama kidete kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini


Askofu mkuu Desmond Tutu wa Kanisa Anglikani, ni kati ya viongozi maarufu sana nchini Afrika ya Kusini, waliosimama kidete kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na matokeo ya juhudi hizi yanaonekana kwa uhuru wa watu wa Afrika ya Kusini ambao kwa sasa wanaendelea kucharuka katika mikakati ya maendeleo endelevu, wakishikamana na kujisikia wamoja na kwamba, tofauti zao za rangi ni utajiri mkubwa wanaopaswa kuupokea kwa heshima na taadhima.

Mfuko wa Mo Ibrahim kwa kutambua mchango wa Askofu mkuu Desmond Tutu, mapema juma hili wamemtunuku Tuzo Maalum kutokana na mchango wake wa kusimamia ukweli, tuzo ambalo linaambatana na kitita cha Dolla za Kimarekani Millioni moja. Askofu mkuu Tutu, kwa miaka mingi tangu ujana wake, alijitoa kimaso maso kutetea: haki msingi za binadamu, utu, heshima, na amani kwa watu wote waliokuwa wanakandamizwa na utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Askofu mkuu Desmond Tutu ni kiongozi ambaye hakuogopa kusema ukweli ambao wakati mwingine unauma kweli kweli. Wakati wa kupokea tuzo hii maalum, Askofu Tutu amesema kwamba, mashujaa wanaopaswa kutuzwa ni wananchi wa Afrika ya Kusini, waliomuunga mkono wakati wa kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Anawakumbuka wapigania uhuru wote waliomtia shime kusonga mbele pasi na kuogopa, wazee walioshirikiana naye kusimamia ukweli na haki msingi za binadamu; wanawake walionesha kwa namna ya pekee tunu bora za kimama bila kumsahau "asali wa moyo wake Mama Leah" ambaye amemwezesha kupata mafanikio aliyo nayo wakati huu.

Mwishoni, Askofu mkuu Desmond Tutu amewakumbusha vijana sehemu mbali mbali za dunia kwamba, ni watu wenye ndoto ya kupata dunia iliyo bora zaidi kwa kuishi, mahali ambapo umaskini utapewa kisogo, ni vijana hawa hawa ambao wako mstari wa mbele kuleta mabadiliko katika mapambazuko mapya yanayoendelea kwenye nchi za Kiarabu. Kwa hakika, vijana ni tumaini la wazee!







All the contents on this site are copyrighted ©.