2012-11-13 10:41:33

Majiundo makini katika taalimungu na tamaduni yataiwezesha mihimili ya Injili kumtangaza Kristo kwa ujasiri mkubwa zaidi


Kardinali Fernando Filoni, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, mapema juma hili amefungua Mwaka wa Masomo 2012 -2013, kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma, kwa Ibada ya Misa Takatifu ili kuomba mapaji ya Roho Mtakatifu.

Wakati wa mahubiri yake, amekumbusha kwamba, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu lipo kwa sababu linapania kukoleza juhudi za kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, hasa zaidi kwa kuyawezesha Makanisa machanga, katika malezi na majiundo makini ya mihimili ya uenezaji Injili katika masomo ya falsafa, taalimungu na kitamaduni, ili vijana wanapohitimu masomo yao wawe wameiva barabara.

Kardinali Filoni ameelezea kwamba, majiundo makini katika tamaduni yanawasaidia wanafunzi hao kuweza kuifahamu historia ya kazi ya ukombozi kwa mataifa yote na kwamba, utume wao kama Mapadre, Watawa na Waamini walei ni huduma kwa Mungu, Kanisa na Jirani.

Mwaka wa Imani uwe ni kikolezo kwa wanafunzi hao kujiandaa vyema kutekeleza wajibu wao ndani ya Kanisa kwa kuunganisha uelewa wao kuhusu Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na historia ya maisha ya mwanadamu mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati sanjari na jitihada za utamadunisho, ili Injili ya Kristo iweze kuota mizizi katika maisha ya mwamini.

Majiundo makini katika taalimungu na tamaduni ni muhimu sana anasema Kardinali Filoni katika jitihada za Mama Kanisa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa. Hii ni huduma nyeti kwa Makanisa mahalia, kwani kama mihimili ya Uinjilishaji wanatumwa na Mama Kanisa kuhubiri, lakini zaidi kutolea ushuhuda wa imani yao kwa njia ya maisha adili na utu wema, kwa kutambua kwamba, wanaendeleza ile kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe yapata miaka elfu mbili iliyopita, katika ulimwengu ambao una mwingiliano mkubwa wa watu kutoka katika kila lugha, kabila na jamaa.

Mwaka wa Imani uwe ni fursa kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Urbaniana kuweza kujishikamanisha na Kristo pamoja na Kanisa lake. Lengo la masomo yao liwe ni kumfahamu vyema Kristo na ujumbe wake, tayari kujitoa kimasomaso kumhubiri hadi miisho ya dunia. Umissionari na dhamana ya kuinjilisha inapata chimbuko lake katika Imani inayoungamwa, inayomwilishwa katika Sakramenti za Kanisa, imani ambayo kimsingi ni dira na mwongozo wa maisha adili yanayopata chimbuko lake katika Amri za Mungu, tayari kuitolea ushuhuda katika sala.







All the contents on this site are copyrighted ©.