2012-11-12 09:01:30

Waraka kuhusu Mahubiri ya Fumbo la Imani unajadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani litakuwa na mkutano wake kuanzia tarehe 12 hadi 15, Novemba 2012, huko Baltimore, pamoja na mambo mengine yanayogusa maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani, wanatarajiwa kupigia kura Waraka kuhusu Mahubiri ya Fumbo la Imani, utakaotolewa na Kamati ya Makleri, Watawa na Miito ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Walengwa wakuu wa Waraka huu ni: Makleri na walezi wa Majando kasisi, ili waweze kutekeleza vyema wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya mahubiri yaliyoandaliwa barabara, yenye kuleta mvuto na mguso; yanayotangaza na kurithisha imani ya Kristo na Kanisa lake. Waraka huu unasema, kiini cha utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu ni Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, atakayerudi kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Wahubiri wanachangamotishwa na Mama Kanisa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba mahubiri yao yanagusa uhalisia wa maisha na kamwe yasiwe ni mahubiri yanayoelea katika ombwe na hivyo kuwaacha waamini wakavu na mahangaiko makubwa katika undani wa maisha yao ya kiroho.

Ni mahubiri yanayopaswa kutambua tofauti za kitamaduni na mwingiliano wa watu, kuliko ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Ni umati ambao unaguswa kwa namna ya pekee na maendeleo ya sayansi na teknolojia bila kusahau tabia ya ukanimungu inayojengeka kwa kasi miongoni mwa Jamii katika nchi zilizoendelea zaidi duniani. Ni waamini ambao kwa kiasi kikubwa hawakubahatika kupata Katekesi ya kina kuhusu mafumbo ya Imani ya Kanisa.

Wahubiri wanapaswa kutambua kwamba, mahubiri yao ni sehemu muhimu sana katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na wala si kiraka katika Ibada zinazoendeshwa na Kanisa, kumbe, kuna haja ya kujiandaa kikamilifu, ili kufikisha ujumbe unaokusudiwa, yaani kuwalisha watu Neno la Mungu, lililoandaliwa vyema, baada ya tafakari ya kina.

Mahibiri yawaguse waamini, ili kuchochea hamu ya kutaka kukutana na Kristo, hamu ya kutaka kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mwana wa Mungu aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa jili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumshikirisha ile hadhi ya kuitwa tena mwana mteule wa Mungu.

Mahubiri yaanzishe mchakato wa majadiliano ya kina kati ya Neno la Mungu na maisha ya mwamini, ili kujenga urafiki wa kweli na Yesu Kristo pamoja na jirani. Wahubiri wawasaidie waamini kuelewa vifungu vya Maandiko Matakatifu mintarafu utamaduni wao, ili kuwajengea uwezo wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, wanapojitahidi kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yawawezeshe waamini pia kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwa na Neno la Mungu wanaposafiri, sehemu zao za kazi lakini zaidi katika familia, ili kweli Neno la Mungu liweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya wafuasi wa Kristo. Wahubiri wajitahidi kuwafahamu vyema waamini wao, ili hata mahubiri yao yaweze kuleta maana na mguso wa kweli, vinginevyo ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa!

Mahubiri yasiwe ni mahali pa Makleri kuonesha umwamba wao katika taalimungu na kwamba, daima wajitahidi kutangaza kile ambacho Mama Kanisa anawataka na wala mahubiri isiwe ni mahali pa kutolea mawazo binafsi. Watambue kwamba, kuna waamini ambao wanashiriki Ibada ya Misa Takatifu hasa zaidi wakati wa Siku kuu ya Noeli, Pasaka, Mazishi, Ndoa na Sakramenti mbali mbali, uwe ni wakati muafaka wa kuwakaribisha tena ili waweze kujisikia kuwa hata wao ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa na kamwe usiwe ni muda wa kuwakejeli na kuwadhalilisha.








All the contents on this site are copyrighted ©.